1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Iran yauonya Umoja wa Ulaya juu ya kuiendelezea vikwazo

15 Septemba 2023

Iran imeuonya Umoja wa Ulaya kwamba uamuzi wake wa kudumisha vikwazo kwa Jamhuri hiyo ya Kiislamu baada ya muda wa mwisho uliowekwa ni "kinyume cha sheria."

Mkuu wa masuala ya nyuklia nchini Iran Ali Akbar Salehi alitangaza Februari 9, 2010 kwamba Tehran imeanza kuzalisha asilimia 20 ya madini ya urani yaliyorutubishwa katika mtambo wake wa Natanz. Picha hii ni ya kinu cha nyuklia cha Bushehr.
Mkuu wa masuala ya nyuklia nchini Iran Ali Akbar Salehi alitangaza Februari 9, 2010 kwamba Tehran imeanza kuzalisha asilimia 20 ya madini ya urani yaliyorutubishwa katika mtambo wake wa Natanz. Picha hii ni ya kinu cha nyuklia cha Bushehr. Picha: Behrouz Mehri/AFP

Wizara ya mambo ya nje ya Iran imesema inauchukulia uamuzi wa Umoja wa Ulaya kama usio halali, wenye nia mbaya na unaokwenda kinyume na makubaliano ya nyuklia.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Uingereza ni kuwa, vikwazo vya Umoja wa Ulaya kwa Iran vitadumishwa. Wizara hiyo imesema uamuzi huo umetokana na hatua ya Iran kutoheshimu masharti ya makubaliano na pia kuendelea na programu yake ya kurutubisha madini ya Urani.

Wizara hiyo imeeleza kuwa, msururu wa vikwazo vya Uingereza, Umoja wa Ulaya na Marekani kwa watu binafsi nchini Iran na mashirika yanayohusika na programu za silaha za nyuklia, vilipaswa kuondolewa Oktoba 18.

Makubaliano kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani mwaka 2015 yalinuia kuzuia mpango wa nyuklia wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu ili kuondolewa vikwazo vya kimataifa.