1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran ina nguvu zaidi kuliko wakati wa vita na Iraq-Rouhani

11 Februari 2019

Rais Rouhani amesisitiza kwamba Iran itaendelea kutengeneza makombora ya aina mbali mbali bila ya hofu na katu hailazimiki kumuomba idhini yoyote kutekeleza azma yake hiyo.

Iran Demonstration 40 Jahre Islamische Republik
Picha: Jamaran

Wairan wako kwenye maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 40 ya mapinduzi ya kiislamu yaliyouangusha utawala wa Shah Mohammed Reza Pahlavi uliokuwa ukiungwa mkono na Marekani.Ujumbe mkubwa uliotolewa na kiongozi wa jamhuri hiyo ya kiislamu umesisitiza kwamba nchi hiyo haitompigia mtu yoyote magoti au kuomba ridhaa ya mtu kuendelea na harakati zake za kujiimarisha kijeshi.

Picha: ISNA

Hotuba ya rais Rouhani imetilia mkazo kwamba njama zinazofanywa na adui dhidi ya Iran zitashindwa kwa namna zote.Na kuonya kwamba sasa nchi hiyo ya Jamhuri ya kiislamu ina nguvu kubwa zaidi kuliko wakati ilipopambana na Saddam Hussein wa Iraq katika vita vilivyosababisha maafa makubwa na uharibifu kutoka mwaka 1980 mpaka 1988.

Rouhani amesema leo hii ulimwengu unapaswa kutambua kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran  ina uwezo mkubwa zaidi kuliko siku za vita. Pia ameipuuza  miito kutoka Marekani na Ulaya  ya kutaka pafanyike makubalino mapya ya kuuzuia mpango wake wa Nuklia.

''Mwaka huu tunasherehekea miaka 40 ya kinachoangaliwa kama siku ya ushindi katika mapinduzi ya kiislamu ya mwaka 1979 ya nchi yetu dhidi ya njama za wahalifu Wamarekani,wazayuni na nchi zilizopitwa na wakati za kanda hii ambazo zinataka kuwaangusha watu wetu  kupitia shinikizo na vikwazo. Leo uwepo wa umma mitaani  katika sherehe hizi za kumbukumbu kote nchini kunamaanisha kwamba njama za maadui zimeshindwa. Uwepo huu unamaanisha kwamba adui hatofanikiwa katika malengo yake ya uovu''

Picha: Mehr

Rouhani pia ameipuuza  miito kutoka Marekani na Ulaya  ya kutaka pafanyike makubalino mapya ya kuuzuia mpango wake wa Nuklia.Lakini kwa upande mwingine Kamanda wa ngazi ya juu katika jeshi la kimapinduzi la Iran amenukuliwa akisema nchi hiyo itaiangamiza kabisa miji ya Israel ya Haifa na Tel Aviv  ikiwa Marekani itaishambilia jamhuri hiyo ya kiislamu. Sambamba na hayo miji mbali mbali ya Iran ilifurika umati wa watu kuanzia Abadan kusiniMagharibi mwa Iran mpaka Mashad kaskazini mashariki mwa nchi hiyo wakisikika wakipaaza sauti za kuilaani Marekani. Kiongozi wa juu wa sasa Ayatollah Ali Khamenei anatajwa kujiandaa kutowa taarifa ya kina yenye malezo kuhusu hatua ya pili ya kuendeleza mapinduzi ya kiislamu.

Mwandishi:Saumu Yusuf /AFP/APE

Mhariri:Josephat Charo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW