Iran: Israel inataka kuiingiza Marekani vitani
15 Januari 2026
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi ameishutumu Israel kwa kutaka kuiingiza Marekani vitani kwa niaba yake. Araghchi ameongeza kuwa la kushangaza, ni kwamba kwa sasa mataifa hayo yamekuwa yakizungumza bayana mambo ambayo awali yalikuwa siri. Wiki hii, Iran imeonya mara kadhaa kuwa iko tayari kufanya mazungumzo na Marekani lakini ikasisitiza pia kuwa imejiandaa kikamilifu kwa vita na kusisitiza kuwa kamwe taifa hilo halijawahi kumruhusu "adui" kufikia malengo yake.
Hali bado ni tete nchini Iran kufuatia maandamano yanayoendelea kusababisha maafa makubwa. Kufikia sasa, waandamanaji 3,428 wameuawa, hii ikiwa ni kulingana na shirika la haki za binadamu la Iran (IHRNGO) lenye makao yake makuu mjini Oslo.
Shirika hilo limesema huenda idadi ya vifo ikawa kubwa zaidi kuliko hiyo iliyotangazwa na kwamba watu zaidi ya 10,000 wamekamatwa na kuelezea wasiwasi wake kufuatia taarifa ya serikali kuwa baadhi ya waliokamatwa watahukumiwa kunyongwa.
Maelfu ya watu wameandamana pia katika miji mbalimbali duniani kudhihirisha mshikamano kwa raia wa Iran. Maryam Palizban ni msanii kutoka Iran aliyeandamana mjini Berlin, Ujerumani:
" Hali ni mbaya. Idadi ya vifo inaongezeka na hatujui kinachoendelea huko kutokana na kuzimwa kwa intaneti. Lakini kila mtu anayewasiliana nasi anatuomba tupaze sauti na kuujuza ulimwengu kuwa damu inamwagika kila mahali na hali ni mbaya zaidi kuliko hapo awali, " alisema muiran huyo anayeishi Ujerumani.
Mzozo wa Iran wazusha hali ya wasiwasi
Marekani imeanza kuwaondoa baadhi ya maafisa wake kutoka kambi muhimu za kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati kama tahadhari, kufuatia mvutano unaoongezeka. Baadhi ya maafisa wa Marekani wameondolewa katika kambi ya Al Udeid huko Qatar, hatua iliyochukuliwa pia na Uingereza. Haya yanajiri baada ya Iran kuonya kuwa itashambulia kambi za Marekani katika mataifa jirani iwapo Washington itaishambulia. Uingereza pia imetangaza kuufunga kwa muda ubalozi wake mjini Tehran.
Rais Donald Trump alisema ataamuru operesheni za kijeshi dhidi ya Iran ikiwa serikali mjini Tehran itaendelea kuwaua na kuwakamata kiholela waandamanaji. Trump aliendelea hivi majuzi kwa kuwataka Wairan kuendelea kuandamana akisema kuwa msaada wa Marekani upo njiani.
Jumatano usiku, Trump amesema amepewa "taarifa zenye kuaminika" kwamba mipango ya serikali ya kuwanyonga waandamanaji waliokamatwa imesitishwa. Hayo ni baada ya utawala mjini Tehran kutangaza kuwa itaendesha haraka kesi za waandamanaji waliokamatwa na kuhukumiwa kifo.