1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran, Israel zaendelea 'kutwangana' vikali

5 Machi 2026

Iran na Israel zimeingia siku ya sita ya mashambulizi makali baina yao, huku Washington ikiendelea kushirikiana na Tel Aviv kuendeleza vita walivyovianzisha kwa mauaji dhidi ya Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatullah Khamenei.

Israel Tel Aviv 2026 | Mashambulizi ya Iran
Sehemu ya madhara ya mashambulizi ya Iran dhidi ya mji mkuu wa Israel siku ya Jumatano (Machi 4,2026).Picha: Abbas Hassan/ZUMA Press/IMAGO

Usiku wa kuamkia Alkhamis (Machi 5) Iran ilifanya mashambulizi makali dhidi ya maeneo mbalimbali nchini Israel, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kijeshi vya Israel na vyombo vya habari vya serikali ya Iran. 

Milio ya ving'ora vya tahadhari ilisikika kote mjini Tel Aviv, ingawa hakukuwa na taarifa kuhusu maafa yaliyosababishwa na mashambulizi hayo yaliyofanyika baada ya ukimya wa takribani masaa saba tangu yale ya mwisho siku ya nyuma yake. 

Jeshi la Israel lilisema limetambua "makombora yaliyorushwa na Iran" kuelekea taifa hilo, huku likidai kuwa mifumo yake ya ulinzi ilikuwa kazini kuyadunguwa makombora hayo.

Halikusema, hata hivyo, ni makombora ya aina gani na mangapi lilifanikiwa kuyadunguwa kati yake. 

Shirika la Utangazaji la Iran (IRIB) liliripoti pia kuhusu mashambulizi hayo.

Jeshi la Israel lilikuwa limewataka raia kutoka kwenye mahandaki yao kwa kuwa "idadi ya makombora yanayorushwa kutoka Iran ilikuwa imepunguwa."

Meli ya mafuta yashika moto Kuwait

Taarifa kutoka Kuwait zilisema mripuko mkubwa umesikikana kwenye pwani ya nchi hiyo na kusababisha kuvuja kwa mafuta.

Shirika linalofuatilia usalama wa vyombo vya baharini la Uingereza (UKMTO) lilisema tukio hilo limetokea kwenye eneo la Mubarak Al-Kabeer. 

Moshi ukifuka baada ya mashambulizi ya Iran dhidi ya Ubalozi wa Marekani nchini Kuwait siku ya Jumatatu (Machi 2, 2026).Picha: AFP

Mripuko huo unatajwa kutokea kwenye meli moja ya mafuta, ingawa haikutajwa sababu ya mripuko wenyewe.

Shirika hilo liliandika kupitia mtandao wa X kwamba "kuna hatari ya kimazingira kutokana na mafuta yanayovuja kutoka kwenye meli hiyo."

Haikujulikana mara moja nani aliyeishambulia meli hiyo, lakini tangu mashambulizi ya Marekani na Israel yalipoanza dhidi yake, Iran imeapa kusababisha hasara kubwa kwenye hatua yake ya kulipiza kisasi uchokozi huo.

Taifa hilo la Kiislamu kwenye Ghuba ya Uajemi limekuwa ikirusha makombora dhidi ya maeneo mbalimbali ya eneo hilo likiyalenga maslahi ya Marekani na washirika wake. 

Kikosi Maalum cha Walinzi wa Mapinduzi kilitangaza siku ya Jumatano kwamba kimeufunga Mlango Bahari wa Hormuz, ujia muhimu ambao asilimia 20 ya mafuta yote duniani hupitia.

Mashambulizi Iraq, Lebanon

Iran pia ilishambulia ndani ya jimbo la Kurdistan kaskazini mwa Iraq, wakati kukiwa na ripoti kwamba Marekani inajaribu kuwatumia wanamgambo wa Kikurdi kupigana vita vyake dhidi ya Tehran.

Iran ilitowa onyo kwa wapiganaji wa Kikurdi kujitenga kando na ushawishi wowote wa kigeni dhidi yake ikidai kwamba ingechukuwa hatua kali kwa yeyote anayehatarisha zaidi usalama wake.

Mashambulizi ya Israel kwenye kijiji cha Khiam siku ya Jumatano (Machi 4, 2026).Picha: Rabih Daher/AFP/Getty Images

Nchini Lebanon nako kuliripotiwa mashambulizi mengine yaliyofanywa na Israel kwenye viunga vya kusini vya mji mkuu, Beirut.

Israel inadai kujibu mashambulizi yaliyofanywa dhidi yake na wanamgambo wa kundi la Hizbullah siku ya Jumatatu (Machi 2), baada ya kundi hilo kusema linalipiza kisasi "mauaji ya kiongozi mkuu wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei."

Tangu wakati huo jeshi la Israel limeyashambulia maeneo kadhaa ya Beirut na limewataka raia kuondoka kwenye maeneo hayo, ambapo zaidi ya watu 50 wameshauawa.

Maseneta wa Republican wakwamisha hoja ya kumzuwia Trump

Nchini Marekani, taifa ambalo linashirikiana na Israel kwenye vita vilivyovianzisha dhidi ya Iran mwishoni mwa wiki iliyopita, maseneta wa chama cha Republican wamefanikiwa kukwamisha rasimu ya hoja ya kuuondolea utawala wa Rais Donald Trump madaraka ya kuendelea na vita vyake hivyo.

Rais Donald Trump wa Marekani amefanikiwa kukiuka kiunzi cha kisheria kwenye vita vyake dhidi ya Iran baada ya wajumbe wa Republican kukwamisha hoja ya kumuondolea nguvu za kuendelea na vita hivyo.Picha: Andrew Caballero-Reynolds/AFP

Hiyo imechukuliwa kuwa ni ishara ya uungaji mkono wa mgogoro huo ambao sasa umeshaenea ukanda mzima wa Mashariki ya Kati kukiwa hakuna dalili kwamba Marekani inajuwa mpango wa kuumaliza.

Rasimu hiyo ifahamikayo kama Azimio la Madaraka ya Vita, ilishindwa kupita kwa kura 47 dhidi ya 53 za walioipinga.

Kwa kiasi kikubwa, kura hiyo ilipigwa kwa misingi ya kivyama, ingawa seneta wa Republican kutoka jimbo la Kentucky, Rand Paul, aliungana na wenzake wa Democrat kuiunga mkono, huku yule wa Democrat kutoka Pennsylvania akiipinga.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW