1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kwa nini Iran inahofia vurugu Afghanistan

27 Oktoba 2021

Msisimko wa awali nchini Iran kuhusu kujiondoa kwa Marekani katika jirani yake wa mashariki anayekumbwa na mzozo umepoa, na hisia sasa zinabadilika. Iran inahofia wita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Afghanistan

Iran Grenzschutz am iranisch-afghanischen Grenzkontrollpunkt in Milak, südöstliche Provinz Sistan-Baluchestan
Picha: Abedin Taherkenareh/dpa/picture alliance

Iran inafanya leo mkutano wa majirani wa Afghanistan pamoja na Urusi ili kujadili hali ya sasa katika nchi hiyo iliyoharibiwa kwa vita. Mkutano huo, ulioandaliwa na Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Iran, unawakutanisha mawaziri wa mambo ya kigeni wa Iran, China, Pakistan, Tajiskistan, Uzbekistan, Tukmenistan na Urusi katika mji mkuu wa Iran, Tehran kuujadili mustakabali wa kisiasa wa Afghanistan na kuundwa kwa serikali mpya. 

Soma zaidi: Taliban yatangaza serikali mpya ya mpito Afghanistan

Kwa mujibu wa televisheni ya Afghanistan ya TOLO News, wawakilishi wa serikali ya Taliban hawajaalikwa. Iran na Afghanistan zinatumia mpaka mmoja wa karibu kilomita 1,000 na Tehran ina maslahi muhimu ya usalama nchini humo. Wairan wengi ni wa madhehebu ya Shia lakini Wasunni walio wachache wanaishi katika maeneo ya karibu na mpaka wa Afgahnistan. Wasunni kwa muda mrefu hulalamika kuhusu kubaguiwa na mamlaka za Iran.

Tangu Taliban ilipochukua madaraka nchini Afghanistan katikati ya Agosti, Iran imekuwa ikijadili kama kundi hilo linalofuata imani kali ya kidini limebadili mbinu zake tang umara ya mwisho lilipokuwa madarakani miaka 20 iliyopita.

Viongozi wa Taliban wakiwa katika mkutano UrusiPicha: Sergei Bobylev/TASS/dpa/picture alliance

Tehran imemtaka jirani yake huyo wa mashariki anayekumbwa na mzozo kuunda serikali inayojumuisha makundi yote ya kisiasa na imara kitu ambacho Iran inazingatia kuwa muhimu kwa ajili ya usalama wake wa kitaifa.

Msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid ameukaribisha mpango huo wa Iran na kuelezea matumaini kuwa matokeo yake yataifaidi Afghanistan.

Soma pia: Urusi yaialika Taliban kwa mazungumzo

Lakini Fatemeh Aman, mtalaamu masuala ya Iran katika Taasisi ya Mashariki ya Kati mjini Washington ameiambia DW kuwa Iran imekosea katika mahesabu. Anasema miundo ya uongozi ya Taliban ina tabaka nyingi, ngumu na isiyoeleweka. Hilo linafanya mazungumzo nao kuwa magumu, na sio tu kwa Iran.

Ndani ya Taliban, hata hivyo, tawi la itikadi Kali – ukiwemo Mtandao wa Haqqani na mahusiano yake imara na Pakistan – linaonekana kushinda. Sirujaddin Haqqani, mtoto wa kiume wa Jalaluddin Haqqani, aliyeanzisha mtandao hi katika miaka ya 1980 wakati wa mapambano ya Afghanistan dhidi ya uvamizi wa Wasovieti, kwa mfano, ndiye waziri mpya wa mambo ya ndani wa Afghanistan.

Haqqani anaaminika kuwa aliyepanga miripuko ya mabomu ya kujitoa muhanga katika miaka 15 iliyopita na yuko kwenye orodha ya Markeani ya FBI ya watu wanaosakwa. Wiki iliyopita, Haqqani alitangaza msaada wa kiuchumi, yakiwemo mashamba ya kilimo, kwa familia za waripuaji wa Kitaliban wa kujitoa muhanga. Mashamba hayo, inaonekana yanaporwa kutoka kwa jamii ya Washia walio wachache.

Soma pia: Umoja wa Ulaya watoa yuro Bilioni moja kuisaidia Afghanistan

Mchambuzi Aman anasema Iran ina wasiwasi mkubwa kuhusu uwezekano wa kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Afghanistan. Ni ngumu kuweka ulinzi kwenye mpaka wao mrefu kwa sababu ya jiografia. Vurugu nchini Afghanistan zinaweza kuweka mazingira ya usafirishaji haramu sio tu wa dawa za kulevya na watu, bali pia silaha kwa maeneo yasiyojiweza.

Ripoti hii ilitafsiriwa kutoka kwa Kijerumani.

 LINK: https://www.dw.com/a-59630081

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi