Iran kuanza tena mazungumzo ya nyuklia
28 Oktoba 2021Naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Ali Bagheri ambaye ndiye mjumbe mkuu wa mazungumzo hayo, amesema Iran imekubali kuanza tena mazungumzo hayo mwishoni mwa mwezi Novemba na tarehe kamili itatangazwa wiki ijayo. Msemaji wa Ikulu ya Marekani Jen Psaki amesema maafisa wa serikali wanafahamu kuhusu matamshi ya Bagheri "Dhamira yetu bado ni kufuata mkondo wa kidiplomasia. Na tunauwachia Umoja wa Ulaya na wapatanishi kuamua ni lini hatua inayofuata itakuwa nzuri."
Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump aliiondoa Marekani kutoka kwenye muafaka wa nyuklia wa 2015 na Marekani imeshiriki katika duru tisa za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja mjini Vienna, ambayo yalilenga kuzirejesha Washington na Tehran katika utekelezwaji wa makubaliano hayo.
Mazungumzo hayo yalisimama tangu Juni wakati Rais wa Iran Ebrahim Raisi alichukua madaraka. Akiwa ziarani Brussels, Bagheri alisema aliona maendeleo katika mazungumzo na mjumbe wa Umoja wa Ulaya Enrique Mora, ambaye pia alikwenda Tehran mapema mwezi huu.
Shirika la Kimataifa la kudhibiti silaha za sumu IAEA limesema Iran inaendelea kisiri kukiuka muafaka huo, uliosainiwa na Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Urusi, China na Umoja wa Ulaya.
Soma pia: IAEA: Iran yarutubisha madini ya kuwezesha kuundwa silaha za nyuklia.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amethibitisha kuanza tena kwa mazungumzo hayo akisema mkuu wa IAEA Rafael Grossi atazuru Iran hivi karibuni. "Kimsingi ziara ya Bwana Grossi nchini Iran katika siku zijazo itafanyika lakini nadhani kusema muda na tarehe sio muhimu. Ni sehemu ya mambo ya kiufundi yanayohusiana na makubaliano ya kiufundi ambayo yatashughulikiwa ili safari ifanyike." Amesema.
Soma zaidi: Iran yaridhia IAEA kuendelea kukagua vituo vya nyuklia
Psaki amesema Marekani na washirika wake bado wanataka suluhisho la kidiplomasia, lakini maafisa wa White House wanasema wanazingatia mbinu nyingine mbadala, ijapokuwa uamuzi utategemea vitendo vya Iran.
Biden anatarajiwa kuelekea Rome baadaye wiki hii kwa mkutano wa kilele wa kundi la nchi 20 tajiri duniani, ambako anatarajiwa kushauriana na washirika kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran pembezoni mwa mkutano huo.
Mshauri wa usalama wa taifa Jake Sullivan alisema watatuma ujumbe wa wazi kwa Wairan, kuwa muda wa kufanya mazungumzo una kikomo.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP