Iran: Marekani haipaswi kuyashurutisha mataifa huru
28 Aprili 2026
Iran imeufunga kabisa ujio huo muhimu wa bahari, tangu Marekani na Israel zilipoanzisha vita vyao dhidi ya Jamhuri hiyo ya kiislamu Februari 28. Vita hivyo hadi sasa vimeathiri pakubwa uchumi wa dunia, kuliyumbisha soko la mafuta na kusababisha nishati hiyo muhimu pamoja na gesi kupanda maradufu.
Njia ya Mlango Bahari wa Hormuz inayotumika kusafirishia asilimia 20 ya mafuta ya dunia pamoja na bidhaa nyengine muhimu, ndio imekuwa jambo gumu kulitatua ili kufikia usitishwaji kamili wa vita na hatimae upatikanaji wa amani kati ya mataifa hayo hasimu.
Iran kwa upande wake kupitia msemaji wa wizara ya Ulinzi Reza Talai Nik, imesema Marekani haina tena nafasi ya kuiamrisha nchi yoyote huru, juu ya nini cha kufanya au hata kuishurutisha kutekeleza sera zake, akisisitiza kuwa ni lazima washington iache kulazimisha mataifa mengine kutii masharti yake aliyoyaita haramu, yasiyokubalika na yaliyokosa uhalisia.
Talai Nik, Akizungumza kuelekea mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Usalama ya Shanghai SCO, amesema pia nchi yake iko tayari kushirikiana na mataifa huru kwa kutoa ushirikiano wao wa kijeshi hasa kwa wanachama wa Jumuiya hiyo.
Marekani haiko tayari kukubali masharti ya Iran
Hata hivyo utawala wa Marekani hauoneshi dalili zozote za kukubali pendekezo jipya kutoka Iran la kumaliza vita na kufungua Mlango huo wa Hormuz. Moja ya masharti ya Iran ni kuitaka Washinton kuahirisha mazungumzo juu ya silaha zake za nyuklia, jambo ambalo Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Marco Rubio, alisema halitowezekana wakati akihojiwa na shirika la habari la Fox News.
"Kwa mara nyengine tena sitobashiri kuhusu uamuzi wa rais katika jambo hili. Inatosha kusema kwamba suala la nyuklia ndilo sababu iliyotufikisha hapa tangu mwanzo. Utawala uliopo hautaki tu kuitawala Iran unataka kuutawala ukanda mzima. Sasa fikiria je wangelikuwa na silaha za nyuklia ingekuwaje. Angalia wanachokifanya katika Mlango bahari wa Hormuz, huo mfano mzuri kabisa. Sasa fikiria kama watu hao hao wangelikuwa na silaha za nyuklia. Watataka kuitawala na kuishikilia mateka dunia nzima,” alisema Marco Rubio.
Kwa sasa Ikulu ya White House imesema Rais wa Marekani Donald Trump hapo jana alikutana na kundi lake la washauri wa usalama wa taifa kutathmini pendekezo hilo kwa makini na baadae Trump atalizungumzia. Pendekezo hilo lilitolewa siku ya Jumatatu wakati wa ziara ya waziri wa mambo ya nchi za nje ya Iran Abbas Araghchi nchini Urusi ambaye ni mshirika wa zamani na muhimu wa Tehran.
Wiki takriban moja iliyopita Iran iliufungua Mlango bahari wa Hormuz baada ya makubaliano kwamba Marekani itaacha kuzingira bandari zake.
lakini muda mfupi baada ya tangazo hilo, Kamandi Kuu ya Jeshi la Iran lilisema Washington imekiuka ahadi ya kufungua kikamilifu shughuli zote za usafirishaji kupitia mlango huo kwa uamuzi wake wa kuendelea na mzingiro wa kijeshi iliyouweka dhidi ya bandari za Iran, ikiwa ni pamoja na kuzuia kuingia na kutoka kwa meli zinazobeba shehena ya mafuta ya Iran.