Iran, Marekani, Israel zasitisha mapigano kwa muda
8 Aprili 2026
Tamko lililotolewa usiku wa kuamkia Jumatano (Aprili 8) na Baraza Kuu la Usalama la Iran liliwashukuru Wairani kwa uvumilivu na kujitolea kwao muda wote wa kushambuliwa na Israel na Marekani, huku pia likiita hatua ya sasa kuwa ni ushindi mkubwa.
"Kwa taifa tukufu, lenye heshima, na shujaa la Iran: Adui ameshindwa kwa kipigo kisichosemeka, cha kihistoria na cha kumvunjavunja kwenye vita vyake haramu na vya kihalifu dhidi ya taifa la Iran." Ilisema sehemu ya tamko hilo lililosomwa kwenye televisheni ya taifa ya Iran.
Baraza Kuu la Usalama la Iran, ambacho ndicho chombo cha juu kwenye masuala ya uongozi nchini humo, liliupongeza umma wa Iran kwa ushindi huo, lakini wakati huo lilisitiza "haja ya uvumilivu na umakini kwa upande wa maafisa na pia ulinzi wa umoja na mshikamano miongoni mwa umma wa Iran" hadi pale kile lilichokiita ushindi "utakapokamilika!"
Tamko hilo lilitolewa muda ule ule ambapo mamilioni ya Wairani walikuwa wamejitokeza kuhami vituo vya umeme, mafuta, majengo ya umma na madaraja, kufuatia kitisho cha Rais Trump kwamba angeliamuru kuripuliwa kwa maeneo hayo usiku wa jana.
Kubadilika kwa Trump
Kwenye ujumbe wake aliokuwa ametuma kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, ambao ulilaaniwa na wakosoaji wake wengi waliouita ushahidi wa "uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari," Trump alikuwa ameandika: "Ustaarabu mzima utakufa usiku wa leo, na hautaweza kamwe kurudi tena ikiwa Iran itashindwa kufikia makubaliano yanayojumuisha kuufunguwa upya Mlango Bahari wa Hormuz."
Lakini wakati dunia ikingojea maangamizo aliyojiapiza kuishushia Iran, Trump alijitokeza tena kwenye mtandao huo huo akitangaza ushindi mwengine na akiwashukuru Waziri Mkuu na Mkuu wa Majeshi wa Pakistan kwa kufanikisha mpango wa usitishaji mapigano wa wiki mbili, uliotokana na pendekezo lenye vipengele 10 la Iran, ambalo awali aliliita "linaloweza kufanyiwa kazi" ingawa baadaye alinukuliwa akiuita "mpango wa ghiliba" bila kufafanuwa.
Israel yakubali lakini yaonya
Mapema asubuhi ya Jumatano, ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ilisema inauunga mkono uamuzi wa Trump wa kusitisha mashambulizi dhidi ya Iran kwa wiki mbili, lakini ikionya kwamba uamuzi huo haujumuishi vita vyake nchini Lebanon, ambako hadi sasa zaidi ya watu 1,500 wameshauwa na zaidi ya milioni moja kuhamishwa makaazi yao.
Hata hivyo, kusitishwa uhasama dhidi ya kile Iran inachokiita "muungano wa mapambano", unaojumuisha makundi ya wapiganaji ndani ya Lebanon, Iraq na Yemen, ni mojawapo kati ya vipengele 10 vya masharti ya Iran kwenye mpango ulioleta usitishaji wa sasa wa mapigano.
Ingawa mpango huo unaweza kuwa msingi wa majadiliano yanayotazamiwa kuanza hapo Ijumaa, una vipengele kadhaa ambavyo awali Washington ilishasema haviwezi hata kujadilika, seuze kutekelezeka.
Kwa mujibu wa mpango huo, Iran inataka iendelea kuudhibiti Mlango Bahari wa Hormuz, iendelee na urutubishaji wa madini ya urani na iondolewe vikwazo vyote vya awali na vya nyongeza.
Vile vile, Iran inaitaka Marekani kuondosha vituo vyake vya kijeshi eneo zima la Mashariki ya Kati, kuziachia mali zake zinazoshikiliwa, na kuwepo kwa azimio maalum la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuyahalalisha na kuyapa nguvu za kisheria makubaliano hayo.