1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran: Mazungumzo ya nyuklia yamefikia hatua muhimu

23 Februari 2022

Iran imesema mazungumzo ya Vienna ya kufufua makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015, yamefikia hatua nyeti na muhimu na nchi za Magharibi zinapaswa kuzingatia hali halisi katika kusuluhisha mambo yaliyosalia.

Iran Tehran | Iranischer Außenminister | Hossein Amir-Abdollahian
Picha: Fatih Aktas/Anadolu Agency/picture alliance

Kauli hiyo aliitoa Waziri wa mambo ya nje wa Iran Hossein Amirabdollahian, katika mkutano na waandishi wa habari na waziri mwenza wa Oman mjini Tehran.

Shirika la habari la Reuters liliripoti wiki iliyopitakwamba makubaliano ya Marekani na Iran yalianza kuchukua muelekeo mwema huko Vienna baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya kufufua Mkataba wa nyuklia uliotelekezwa mnamo mwaka 2018 na Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye pia aliiwekea tena vikwazo vikubwa Iran.

Kikao cha mazungumzo ya nyukliaPicha: EU Delegation in Vienna/Handout/AFP

Iran haitovuka mstari wake mwekundu

Mkataba wa mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani uliiwekea mipaka Tehran katika mpango wake wa urutubishaji wa urani ili iwe vigumu kuendeleza nyenzo kwa ajili ya silaha za nyuklia, na hilo lilipelekea kuondolewa vikwazo vya kimataifa dhidi ya Tehran.

Amirabdollahian amesema Iran imemsisitizia Mwanadiplomasiamkuu wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell, wakati Mkutano wa kila mwaka wa Usalama uliofanyika mjini Munich Ujerumani, kwamba Tehran kamwe haitavuka mstari wake mwekundu wakati wa mazungumzo hayo huku akikemea hatua za NATO na Marekani.

Mazungumzo yanaelekea kukamilika

"Tabia ya uchochezi ya NATO na Marekani imezua hali ya sintofahamu katika eneo hilo, ambalo liko kaskazini mwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Tunahimiza pande zote kukomesha mgogoro huu kwa njia za kisiasa na za amani," alisema Hossein.

Kiongozi wa majadiliano ya nyuklia wa Iran akiondoka ViennaPicha: Askin Kiyagan/AA/picture alliance

Mjumbe wa Urusi amesema Jumanne hii kuwa mazungumzo yanakaribia kumalizika, na vyanzo vilivyo karibu na mazungumzo hayo vimeeleza kuwa mpango wa kubadilishana wafungwa kati ya Iran na Marekani unatarajiwa hivi karibuni.

Tangu mwaka 2019, kufuatia kujiondoa kwa Marekani katika mpango huo, Tehran imekwenda mbali zaidi na kukusanya upya akiba ya urani iliyorutubishwa, na kuisafisha kwa kiwango cha juu na pia kuweka miundombinu mbadala ili kuongeza kasi ya uzalishaji wa nishati hiyo.