Mazungumzo kati ya Iran na Marekani yapo njia panda
27 Machi 2026
Iran na Marekani bado zipo njia panda kuhusu suala zima la kumaliza vita vya Mashariki ya Kati huku kila upande ukionekana kusalia na msimamo wake kuhusu mazungumzo ya kusitisha mapigano, jambo linalotishia mzozo huu kuongezeka hasa ikiarifiwa kuwa maelfu ya wanajeshi wa Marekani wanakaribia eneo hilo.
Hata hivyo, mjumbe maalum wa rais wa Marekani Steve Witkoff amesema kuna "ishara za wazi" kuwa Tehran wako tayari kujadiliana , huku shirika la habari la Iran Tasnim likiripoti kuwa jibu la Iran kwa pendekezo la Marekani lilitumwa rasmi jana usiku kupitia wapatanishi, na kwamba kwa sasa Tehran inasubiri jibu.
Afisa wa Iran ambaye hakutaka kutajwa jina amesema miongoni mwa mashari ya Iran ni kudai fidia kutokana na uharibifu uliosababishwa na vita na kwamba uhuru wa Iran kuhusu Mlango-Bahari wa Hormuz ni lazima uheshimiwe, matakwa ambayo amesema hayakuwemo kwenye mpango huo wa Marekani.
Mashambulizi ya kila upande yaendelea
Ving'ora vilisikika huko Israel vikitahadharisha kuhusu mashambulizi ya makombora ya Iran, huku mataifa ya Ghuba yakipambana kuzuia makombora na droni ya Iran ambayo pia imeendelea kushambuliwa na Israel na Marekani.
Aidha, Rais Donald Trump ametangaza kurefusha muda wa onyo alilolitoa kwa Iran hadi Aprili 6 ili iwe imeufungua Mlango-Bahari wa Hormuz tofauti na hivyo ataishambulia vikali miundombinu ya nishati, lakini Tehran imeimarisha udhibiti wake kwenye njia hiyo muhimu ya baharini. Trump amesema amechukua uamuzi huo kufuatia ombi la Tehran na akaongeza kuwa mazungumzo yanaendelea vyema.
Israel pia imepeleka wanajeshi zaidi kusini mwa Lebanon ili kupambana na kundi la wanamgambo la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran, ambapo mapigano ya Alhamisi yalisababisha hasara kwa pande zote mbili huku Lebanon ikisema itawasilisha malalamiko kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufuatia mashambulizi ya Israel.