1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Iran na Marekani kuendeleza mazungumzo Uswisi

16 Februari 2026

Mazungumzo kati ya Marekani na Iran yatafanyika tena wiki hii mjini Geneva. Iran imesema iko tayari kubadili msimamo wake kuhusu nyuklia ikiwa Marekani itaondoa vikwazo.

Oman | Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi (kushoto) akiwasili Muscat
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi (kushoto) akiwasili Oman wakati wa duru ya kwanza ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani: 11.05.2026Picha: IRANIAN FOREIGN MINISTRY/Handout/AFP

Taarifa ya kuanza kwa duru hiyo ya pili ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Marekani na Iran ilitolewa baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi kusafiri jana Jumapili kuelekea mjini Geneva nchini Uswisi kuhudhuria mazungumzo hayo.

Kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, majadiliano hayo yatafanyika siku ya Jumanne chini ya upatanishi wa Oman, na kwamba suala kuu litakalojadiliwa ni mpango wa nyuklia wa Iran.

Araghchi anatarajiwa kukutana na maafisa wa kimataifa na wale wa serikali ya Uswisi na Oman. Atakutana pia na mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la kudhibiti matumizi ya nyuklia (IAEA), Rafael Grossi.

Marekani kwa upande wake itawakilishwa na mjumbe wa rais Donald Trump Steve Witkoff na mkwewe Trump, Jared Kushner ambao pia wameelekea mjini Geneva. Siku ya Jumapili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alisisitiza kuwa Washington bado ina nia ya kupata suluhisho la kidiplomasia na  kumaliza tofauti zake na Tehran.

Wito wa Israel wa kusambaratisha uwezo wa Iran

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Picha: Debbie Hill/UPI Photo/IMAGO

Kabla ya mkutano huo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametoa wito wa "kusambaratisha kabisa" uwezo wa Tehran kurutubisha madini ya urani. Netanyahu amesema ikiwa makubaliano yatafikiwa, yanapaswa kuwa na vipengele kadhaa ambavyo tunaamini ni muhimu si tu kwa usalama wa Israel, bali kwa usalama wa  Marekani  na dunia nzima.

" Kwanza, madini yote ya urani yaliyorutubishwa ni lazima yaondoke Iran. Jambo la pili ni kwamba haipaswi kuwa na uwezo wa urutubishaji, na sio tu kusitisha mchakato huo bali kuvunja vifaa na miundombinu ya urutubishaji. Na jambo la tatu ni kushughulikia pia masuala ya makombora ya masafa marefu," alisisitiza Waziri Mkuu huyo wa Israel.

Israel na mataifa ya Ulaya yamekuwa yakiishtumu Iran kuwa na mpango wa kumiliki silaha za nyuklia, madai ambayo Tehran imekuwa mara kadhaa ikiyakanusha na kusisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni kwa ajili ya matumizi ya kiraia.

Iran  kwa upande wake imesema iko tayari kubadili msimamo wake kuhusu madini yake ya Urani yaliyorutubishwa ikiwa vikwazo vya kiuchumi vya Marekani vitaondolewa. Kauli hiyo imetolewa na naibu waziri wa mambo ya nje wa Iran Majid Takht-Ravanchi.

Matamshi ya Takht-Ravanchi yanafuatia kurejea kwa mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na Marekani mnamo Februari 6 nchini Oman, huku duru ya pili ikipangwa kufanyika Uswisi siku ya Jumanne.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW