Iran na Marekani kujadili mkataba wa nyuklia Vienna
6 Aprili 2021Tangazo lililotolewa Ijumaa kwamba Marekani na Iran wataanza mazungumzo hayo ndiyo ilikuwa mojawapo ya ishara za kwanza kuhusiana na hatua zinazopigwa kuhakikisha kwamba nchi hizo zinarudi katika kuyatimiza masharti ya mkataba huo ambao ambao unaiwekea Iran mipaka katika masuala ya nyuklia na iwapo itatii basi itapunguziwa vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa na Marekani na jamii ya kimataifa.
Huku Iran ikiwa imekanusha mara kadhaa kwamba haitaki mazungumzo ya aina yoyote na Marekani, Marekani imesema inatarajia mazungumzo hayo yasiwe rahisi na kwamba hakutokuwepo na muafaka wa mapema.
Iran inatilia shaka kupatikana kwa mwafaka
"Hatuna matumaini na vile vile hatuezi kukosa matumaini kuhusiana na matokeo ya mkutano huu kwa sasa lakini tuna imani kwamba tuko katika njia sahihi na iwapo nia ya Marekani na uaminifu wake utathibitishwa, hii huenda ikawa ishara nzuri kwa ya mustabali mwema kwa makubaliano haya na hatimaye utekelezwaji wake kikamilifu," alisema Ali Rabei, msemaji wa serikali ya Iran.
Afisa mmoja wa Iran alisikika akitilia shaka zaidi uwezekano wa kupatikana maelewano katika mazungumzo hayo alipowaambiwa waandishi wa habari wa shirika la Reuters kwamba, "ajenda yetu kwenye mkutano huo itakuwa kuondolewa kwa vikwazo vyote vya Marekani dhidi ya Iran, kama alivyosema kiongozi wetu mkuu mara kadhaa, kitu chochote mbali na hilo, hakitokubalika na Iran."
Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ambaye anatoa kauli ya mwisho kuhusiana na masuala yote ya kitaifa amepinga hatua yoyote ya kuvipunguza hatua kwa hatua vikwazo dhidi ya Iran.
Iran imekuwa ikikiuka masharti ya mkataba wa nyuklia
Mwanadiplomasia mmoja wa nchi za Magharibi aliliambia shirika la habari la Reuters Ijumaa kwamba, kutatumika mbinu ya nchi ya tatu kuyasimamia mazungumzo hayo ambapo Ufaransa ndiyo itakayochukua jukumu hilo.
Iran imekuwa ikikiuka sana masharti ya mkataba huo wa nyuklia kama kiasi cha madini ya urani inachoweza kuhifadhi na kiasi ambacho inaweza kuyarutubisha. Hatua hii inasemekana ni njia ya Iran kuziwekea shinikizo nchi zengine katika mkataba huo kama Urusi, Ujerumani, Ufaransa, China na Uingereza kuongeza juhudi kwa ajili ya kuondolewa vikwazo vinavyoilemaza Iran vilivyowekwa na rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.
Rais Joe Biden aliingia madarakani akisema kuirudisha Marekani katika mkataba huo wa nyuklia lilikuwa mojawapo ya malengo yake muhimu ila Iran na Marekani hawakubaliani kuhusiana na matakwa ya Iran ya vikwazo kuondolewa kwanza.