1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran na Nigeria zatoka sare tasa

17 Juni 2014

Iran na Nigeria zilitoka sare ya bila kufungana goli katika mchuano wao wa kwanza wa Kombe la Dunia. Iran walionekana kuegesha basi kutoka mwanzo, wakati Nigeria wakishindwa kuona lango la mpinzani.

Fußball WM 2014 - Iran Nigeria
Picha: picture-alliance/dpa

Baada ya mechi 12 za magoli ya kusisimua, na vituko uwanjani, mchuano wa 13 haukuwa na chochote cha kuvutia. Mambo yalikamilika sifuri kwa sifuri katika mchuano baina ya Iran na Nigeria mjini Curitiba.

Vijana wa Iran wake kocha Carlos Queiroz walionekana kama wenye uwezo wa kupata ushindi wa goli moja kwa sifuri matokeo ambayo waliyasajili sana katika safari yao ya kufuzu katika Kombe la Dunia, na dhidi ya Nigeria, mpango wao ulikuwa ni ule ule.

Bila kuwa na wachezaji nyota, Iran walicheza kwa kuutumia mfumo wa kujikinga sana hali iliyowafanya vijana wa Super Eagles kushindwa kubuni kitu chochote kaunzia katika safu ya kiungo.

Mshambuliaji wa Nigeria Emmanuel Emenike alishindwa kutikisa mara kadhaa nyavu za mpinzaniPicha: picture-alliance/dpa

Lakini vijana wa Stephen Keshi, Nigeria wanastahili kubeba lawama ya matokeo hayo wao wenyewe. Walishindwa kutikisa wavu licha ya kuwa waliumiliki mpira kwa uzuri. Goli la dakika ya nane lililopachikwa wavuni na Nigeria lilikataliwa na refarii baada ya John Obi Mikel kusemekana kumchezea rafu mlinda lango wa Iran.

Kiungo wa Nigeria John Obi Mikel alisema “walikuwa na watu 11 nyuma ya mpira, hali iliyofanya iwe vigumu kwetu kutengeneza nafasi za kufunga magoli“. Kocha wake Stephen Keshi alisema timu yake ilijawa na wasiwasi baada ya kushindwa kupenya katika ngome ya Iran.

Nafasi pekee kwa kila timu kuweza kupenya katika kundi hilo ni kuipiku Bosnia-Herzegovina, kwa sababu Argentina ndio inayopigiwa upatu kuongoza kundi hilo.

Kocha wa Iran Carlos Queiroz alisema matokeo hayo yalikuwa “mazuri” na kwamba vijana wake walistahili “huruma na heshima” kwa kucheza katika dimba kubwa licha ya athari za vikwazo vya kiuchumi dhidi ya nchi yake, hali iliyofanya mambo kuwa magumu katika kuandaa mechi za kirafiki.

Mreno huyo aliongeza kuwa “bila shaka watu wangewataka wafunge magoli manne au matano, lakini kwao wanaonelea afadhali waende nyumbani na pointi moja“. Anasema timu yake haina wachezaji kutoka Liverpool, Chelsea na Lazio. Kwa hivyo wachezaji wake walisherehekea kazi yao ngumu, uvumilivu na mtazamo waliokuwa nao.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Mohammed AbdulRahman