1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Iran na Pakistan kuimarisha uhusiano wao wa kibiashara

22 Aprili 2024

Rais wa Iran, Ebrahim Raisi, na Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif, wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wao wa kiuchumi na kiusalama. Haya yamejiri baada ya Raisi kufanya ziara ya siku tatu mjini Islamabad.

Ebrahim Raisi na Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif
Rais wa Iran Ebrahim Raisi, akiwa na Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif mjini Islamabad katika ziara yake hukoPicha: Uncredited/Prime Minister Office/AP/dpa/picture alliance

Mkutano wa viongozi hao wawili ni sehemu ya juhudi za kufufua mahusiano yao, yaliyoingia doa mapema mwezi Januari wakati wanajeshi ya nchi zao waliposhambuliana wakiwalenga wanamgambo waliodaiwa kushambulia kila upande. 

Mkutano huo pia unafanyika wakati nchi hizo mbili za Kiislamu zikiwa na lengo la kuimarisha mahusiano yao, baada ya mashambulizi ya kijeshi ya kulipiziana kisasi kati ya Israel na Iran. Ofisi ya Ibrahim Raisi imesema pande zote mbili zimeridhia kuongeza biashara ya nchi hizo mbili kwa miaka mitano ijayo. Kutokana na hilo, mikataba minane ya kibiashara ilitiwa saini kati ya nchi hizo. Walijadili pia kuhusu mpango wa nishati ya gesi uliokwama mwaka 2014 kufuatia Marekani kuupinga na kusema unakiuka vikwazo iran ilivyowekewa kufuatia mpango wake wa nyuklia.

Rais wa Iran kuizuru Pakistan kusawazisha mivutano

Mpango huo ulikuwa usafirishe gesi ya Iran kwa maeneo kadhaa nchini Pakistan. Viongozi hao wawili pia wamekubaliana kushirikiana katika kutatua changamoto za pamoja ikiwemo kitisho cha ugaidi. Raisi pia alikutana na Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Pakistan Ishaq Dar na kujadili kwa kina kuhusu maendeleo ya kikanda na kidunia  na kuthibitisha kushirikiana kutatua changamoto za kikanda.

Wakati ziara ya Raisi nchini Pakistan ikiangaliwa kama hatua muhimu kuelekea kuimarisha mahusiano na Pakistan, kiongozi wa juu kabisa nchini Iran Ayatollah Ali Khamenei, ambaye sio raisi wa taifa hilo ndiye aliye na usemi wa mwisho juu ya masuala ya taifa ikiwemo sera za mpango wake wa nyuklia.

Mzozo wa Mashariki ya Kati wajadiliwa katika ziara ya Raisi

Bendera ya Iran na Israel mataifa yanayohasimiana Picha: H. Tschanz-Hofmann/IMAGO

Huku hayo yakiarifiwa hali imezidi kuwa ya wasiwasi katika kanda ya Mashariki ya Kati, baada ya Iran kuishambulia Israel wiki moja iliyopita na Israel nayo kuishambulia Iran siku ya Ijumaa. Awali Pakistan iliyomba nchi hizo mbili zinazohasimiana kuvumiliana na kuzuwiya mzozo kutanuka nakuingia katika mataifa mengine ya kanda hiyo.

Mripuko wauwa mmoja, wajeruhi wanane Iraq

Katika mazungumzo ya Raisi na Shehbaz Sharif pia mzozo wa Mashariki ya Kati uligusiwa, ambapo Waziri Mkuu huyo wa Pakistan alisifia Iran kwa kuchukua msimamo juu ya hali mbaya ya kibinaadamu Gaza na kutaka kukomeshwa mara moja kwa mateso ya watu wa Palestina. Ameyatolea mwito pia Mataifa ya Kiislamu kuungana na kupaza sauti zao kutaka mzozo kati ya Israel na Hamas kusitishwa haraka.

Raisi, aliyeandamana na ujumbe uliomjumuisha waziri wake wa mambo ya kigeni, Hossein Amir-Abdollahian pamoja na mawaziri wengine atautembelea pia mji wa Mashariki wa Lahore na mji wa bandari wa Karachi ulioko upande wa kusini mwa Pakistan.

reuters/ap