1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran na Saudi Arabia zaendelea na urekebishaji wa mahusiano

11 Novemba 2024

Baada ya miongo kadhaa ya uhasama, Iran na Saudi Arabia zimeelewa kwamba ni katika maslahi yao ya pamoja kurekebishwa uhusiano wao. Hata hivyo yapo masuala kadhaa ya mvutano yanayosalia.

Mkutano kati ya Iran na Saudi Arabia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi alikuwa mjini Riyadh mwezi OktobaPicha: ISNA

Iran na Saudi Arabia zinaendelea na urekebishaji wa tahadhari wa mahusiano yao baada ya makubaliano yaliyosimamiwa na China mwaka 2023. Ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, mjini Riyadh mwezi Oktoba na mkutano wake na Mrithi wa Kiti cha Ufalme Mohammed bin Salman inaashiria kuimarika kwa uhusiano.

Soma pia: Viongozi wa Kiarabu na Kiislamu wakutana Saudia kujadili mzozo wa Mashariki ya Kati

Mabadiliko haya ni hatua muhimu kutoka mivutano ya muda mrefu inayotokana na tofauti za kidini na kisiasa tangu mapinduzi ya Iran ya mwaka 1979. Kwa muda mrefu, Iran imekuwa ikijiona kama kiongozi wa Waislamu wa madhehebu ya Kishia na harakati za mapinduzi, huku Saudi Arabia, chini ya utawala wa kisunni, ikijiona kama kiongozi wa eneo hilo kwa nafasi yake kama mlinzi wa maeneo matakatifu ya Kiislamu ya Mecca na Madina.

Misimamo tofauti kati ya Iran na Saudi Arabia ilidhihirika wakati wa maandamano ya mataifa ya Kiarabu mwaka 2010, ambapo Saudi Arabia ilihofia kuwa Iran ingetumia maandamano hayo kwa faida yake. Licha ya kauli za marishiano, nchi hizo zinaendelea kukabiliana nchini Yemen, ambako zinaunga mkono pande hasimu za mzozo nchini humo.

Saudi Arabia inajiweka katika mstari wa mbele kutafuta suluhisho katika mzozo wa mashariki ya katiPicha: Saudi Press Agency/APA/ZUMA/picture alliance

Wakati Iran inawaunga mkono Wahouthi, Saudi Arabia inaongoza muungano wa kijeshi unaoundwa na mataifa ya Kisunni, ambao pia unaungwa mkono na mataifa ya Magharibi, hasa Marekani, kupambana nao. Moja ya malengo makuu ya muungano huo lilikuwa kurejesha nyuma ushawishi wa Iran.

Soma pia:Iran yasema Saudi Arabia imewafukuza waandishi habari 6 wa televisheni ya taifa ya Iran

Sebastian Sons, kutoka taasisi ya ushauri ya CARPO yenye makao yake mjini Bonn, anaamini maridhiano hayo yana faida kubwa kwa matazamo wa Saudi Arabia. Baada ya shambulio la Iran dhidi ya vituo vya mafuta vya Saudi mwaka 2019, Riyadh iligundua kuwa haiwezi kuitegemea kikamilifu Marekani na hivyo kuona haja ya kutatua masuala yake na jirani yake Iran.

Kwa Riyadh, utulivu wa kikanda ni muhimu kwa mafanikio ya uchumi wao unaotegemea mafuta. Pia, Saudi Arabia inataka kumaliza mgogoro wa Yemen na kusitisha mashambulizi ya Wahouthi dhidi ya ardhi yake, ikitumaini kuwa Iran inaweza kuwashawishi Wahouthi kupunguza vurugu.

Uchambuzi huu unaonyesha mabadiliko katika siasa za Mashariki ya Kati, ambapo Iran na Saudi Arabia zinaendelea kurekebisha uhusiano wao kwa kuzingatia maslahi yao ya kimkakati. Hata hivyo, Hamidreza Azizi, kutoka taasisi ya masuala ya kimataifa na usalama ya SWP ya mjini Berlin, anasema bado haiko wazi ni ushawishi kiasi gani ilio nao Iran kwa Wahouthi.

Iran yasema mashambulizi ya Houthi dhidi ya Saudia ni onyo

00:58

This browser does not support the video element.

Aliiambia DW kuwa haiwezekani kwa Iran kuwaamuru Wahouthi kwa kila hatua wanayochukua. Lakini aliongeza kuwa Iran na Wahouthi wanazingatia maslahi ya kila mmoja, na hilo linaweza kuchangia juhudi za kusitisha vita zinazoendelea nchini Yemen.

Kwa sababu ya vikwazo vya kiuchumi na changamoto za ndani, Iran inaona hatua hii kama njia ya kuimarisha usalama wake huku ikitafuta nafasi katika mashirika ya kimataifa kama BRICS na Shirika la Ushirikiano la Shanghai.

Kwa upande mwingine, Saudi Arabia inataka kujijengea nafasi kama mpatanishi wa kikanda huku ikiendeleza uhusiano mzuri na Marekani na Israel. Kulingana na Guido Steinberg, nchi hiyo inasisitiza kuwa haina lengo la kuachana na washirika wa Magharibi bali kutafuta uhuru wa kimkakati.

Saudi Arabia, kama Qatar, inatumia nafasi yake kutuma ujumbe kati ya Marekani na Iran, na inaonyesha nia ya kudumisha amani kwa kuendelea kuwa na mawasiliano ya wazi na Tehran.

Azizi ana matazamo sawa. Anadhani kwamba uhusiano ulioboreka kati ya Iran na Saudi Arabia huenda ukachangia utulivu wa muda mrefu wa kanda hiyo, na kwamba Tehran imeelewa kwamba maridhiano yako katika maslahi ya pande zote mbili.