Iran na Urusi kuanza luteka ya pamoja ya kijeshi
18 Februari 2026
Shirika la habari la Fars limeripoti hilo siku chache baada ya Kikosi Maalum cha Walinzi wa Mapinduzi Iran, kufanya luteka ya kijeshi katika mlango wa bahari wa Hormuz.
Kamanda wa jeshi la wanamaji la Iran Hassan Maghsoodloo amesema luteka hiyo ina lengo la kuunda nguvu za pamoja na uratibu wa hatua za pamoja kukabiliana na hatua zinazotishia usalama wa majini na usalama wa nchi hizo mbili. Ameongeza kuwa mazoezi hayo ya kijeshi pia yananuia kupambana ugaidi.
Hatua hizi zinajiri baada ya Marekani kutishia kuivamia kijeshi Iran kufuatia kile ilichosema kuwa Jamhuri hiyo ya kiislamu inatekeleza mauaji dhidi ya waandamanaji na pia imeshindwa kufikia makubaliano kuhusu silaha zake za Nyuklia.
Maafisa wa Iran wamekuwa wakitishia kuufunga mlango bahari wa Hormuz hasa wakati wa mvutano kati yake na Marekani, lakini hadi sasa haijawahi kuifunga lango hilo la bahari.