1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran na Uturuki zafanya mazungumzo juu ya Syria

7 Agosti 2012

Mwakilishi mmoja wa kiongozi wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, amefanya ziara ya ghafla nchini Syria kwa ajili ya mazungumzo na Rais Bashar al-Assad katika wakati ambao mapigano nchini humo yanaendelea.

Saeed Jalili, mwakilishi wa Ayatollah Khamenei
Saeed Jalili, mwakilishi wa Ayatollah KhameneiPicha: AP

Saeed Jalili, ambaye pia ni mkuu wa baraza la usalama la Iran, aliwasili Syria mapema Jumanne, akitokea Beirut, mji mkuu wa Lebanon. Huko alikuwa na mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo. Iran, ambayo ni mshirika mkuu wa Syria, imekuwa ikikosoa ushirikiano unaotolewa na nchi kama Marekani, Uturuki, Saudi Arabia na Qatar kwa waasi wanaopamabana na vikosi vya Assad. Mbali na hayo, Iran ina wasiwasi juu ya hatma ya raia 48 wa nchi hiyo, waliotekwa na waasi mwishoni mwa wiki iliyopita.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Ali Akbar Salehi, atafanya ziara nchini Uturuki Jumanne kufanya mazungumzo juu ya mzozo wa Syria na juu ya kisa cha raia hao 48 wa Iran waliotekwa. Mwanadiplomasia mmoja wa Uturuki amelieleza shirika la habari la AFP kwamba Salehi atakutana na mwenzake wa Uturuki, Ahmet Davutoglu na watajadili zaidi kuhusu mzozo wa Syria.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Ali Akbar SalehiPicha: Reuters

Nchini Syria kwenyewe, mapigano yanaripotiwa kuendelea katika mji wa Aleppo uliopo kaskazini mwa nchi hiyo. Majeshi ya serikali leo yameendelea na juhudi zake za kuteka maeneo ambayo sasa yanakaliwa na waasi. Wapigananaji wasiopungua 25 wameuwawa katika machafuko yaliyotokea leo. Mauaji hayo yalitokea baada ya waasi kukishambulia kituo cha kuzalisha umeme na hivyo, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya taifa, kuwalazimisha wanajeshi wa serikali kuwashambulia waasi na kuuwa 25 kati yao.

Idadi ya wakimbizi yaongezeka

Waasi wanadai kwamba wamefanikiwa kukiteka kituo cha ukaguzi wa kijeshi kilichopo kaskazini mashariki mwa Aleppo. Akizungumza na shirika la habari la dpa kwa njia ya simu, kamanda wa jeshi huru la Syria, Abu Omar al-Halabi, alisema kwamba waasi walifanikiwa kuteka kituo hicho baada ya kupambana na vikosi vya Assad kwa muda wa masaa 10. Kwa sababu ya kuendelea kwa machafuko, Umoja wa Mataifa umeamua kuwaondoa waangalizi wake katika mji wa Aleppo. Waangalizi hao sasa wamepelekwa kwenye mji mkuu wa Syria, Damascus.

Uharibifu uliosbabishwa na vita mjini AleppoPicha: Reuters

Machafuko yanayoendelea Syria yanasababisha wimbi la wakimbizi kuongezeka. Zaidi ya raia 1,000 wa nchi hiyo, akiwemo jenerali mmoja wa jeshi, wamekimbilia Uturuki wiki hii. Hadi sasa, inakadiriwa kwamba idadi ya wakimbizi kutoka Syria waliopo Uturuki imefikia 50,000. Jenerali aliyekimbilia Syria leo anasemekana kuambatana na maafisa wengine 12 wa jeshi.

Hata hivyo, utawala wa Uturuki umekataa kutoa idadi kamili ya majenerali walioukimbia utawala wa Assad na waliopo Uturuki hivi sasa. Baadhi yao wanaripotiwa kurudi Syria na kujiunga na waasi katika juhudi za kumwondoa Assad madarakani.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW