1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege ya Ukraine huenda ilipata tatizo kabla kuanguka

9 Januari 2020

Serikali ya Iran imesema ndege ya Ukraine iliyoanguka nje kidogo ya mji wa Tehran na kusababisha vifo vya watu wote 176 waliokuwemo ndani, iligeuka kutaka kurejea ilikotoka baada ya kuwa na tatizo.

Iran Ukrainisches Passagierflugzeug nahe Teheran abgestürzt
Picha: Reuters/WANA/N. Tabatabaee

Canada na Marekani zimetaka uchunguzi kamili ufanyike ili kubaini chanzo cha ajali hiyo iliyotokea juzi, muda mfupi baada ya Iran kurusha makombora kwa wanajeshi wa Marekani nchini Iraq kama majibu ya kuuwawa  kwa kamanda wake wa juu wa jeshi nchini humo Qassem Souleimani katika shambulio lililofanyika mjini Baghdad.

Hata hivyo, hapakuwa na ishara ya wazi kuwa majibu hayo ya kulipiza kisasi ndio sababu ya ndege ya shirika la ndege la Ukraine UIA kuanguka muda mfupi baada ya kupaa angani.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kwa upande wake ameonya dhidi ya kueneza uvumi juu ya sababu za kuanguka kwa ndege hiyo, lakini wakati huo huo akisema ndege za Ukraine hazitaruhusiwa kupaa katika anga za Iraq na Iran:

Rais Zelensky ameongeza kuwa, wataalamu wa anga 45 kutoka Ukraine, na maafisa wa usalama wameondoka leo kwenda Iran kujiunga na kundi la uchunguzi, pamoja na kukikagua kisanduku cheusi kilichopatikana na Iran katika eneo la tukio. Maafisa wa usalama wa Ukraine wamesema wachunguzi wanazingatia sababu saba zinazoweza kuwa chanzo cha ajali hiyo.

Oleksiy Danilov, Katibu wa baraza la usalama wa kitaifa na ulinzi nchini Ukraine amesema sababu hizo zinaweza kuwa kugongana na kitu kingine hewani, roketi kutoka mfumo wa ulinzi wa makombora wa Iran, kuripuka kwa injini kulikosababishwa na sababu za kiufundi na hata mripuko ndani ya ndege hiyo kufuatia sababu ya kiugaidi. Lakini amesema kwa sasa hakuna sababu ya kuamini kuwa ndege hiyo ilishambuliwa kwa roketi.

Iran yasema haitopeleka kijisanduku cheusi kwa Marekani

Picha: picture-alliance/dpa/MAXPPP/Le Pictorium/S. Souici

Huku hayo yakiarifiwa, mkuu wa mamlaka ya ndege ya Iran, Ali Abedzadeh, amesema nchi yake itashirikiana na Ukraine katika uchunguzi lakini haitokipeleka kisanduku cheusi Marekani, ambayo haina na mahusiano nayo ya kidiplomasia kwa miongo kadhaa sasa.

Kulingana na wataalamu wa masuala ya anga ni mataifa machache yenye uwezo wa kufanyia uchunguzi kijisanduku cheusi kinachotoa habari ya kile kilichotokea katika ndege kabla ya kupata ajali. Mataifa hayo ni pamoja na Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Marekani. Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau, amesema serikali yake itahakikisha kunakuwa na uchunguzi huru na masuali ya raia wake kujibiwa.

Kulingana na ujumbe ulioandikwa na mamlaka ya ndege ya Iran katika tovuti yake, ndege hiyo iliokuwa inaelekea upande wa magharibi ili iondoke katika eneo hilo la uwanja wa ndege iligeukia upande wa kulia  na kurejea katika uwanja huo wa ndege baada ya kugundua kuwa kuna tatizo kabla ya kuanguka.

Raia 82 kutoka Iran, 63 kutoka Canada, Waswissi 10, Waafghani 4, Wajerumani watatu na Waingereza watatu, raia 11 wa Ukraine na wafanyakazi 9 wa ndege hiyo ni miongoni mwa waliangamia katika ajali  ya ndege hiyo chapa Boeing 737.

Chanzo:/AFP/dpa