Iran Nyuklia
13 Novemba 2010Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton, amepokea ombi kutoka kwa mpatanishi mkuu wa masuala ya nyuklia wa Iran, Saeed Jalili, la kukutana mapema mwezi ujao kujadili mpango wa nyuklia wa Iran. Wiki hii,Jalili alimuandikia Ashton barua kupendekeza kukutana mjini Istanbul.Baada ya kushauriana na mataifa sita makuu duniani, yatakayowakilishwa na Ashton yaani, Marekani, Urusi, China, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani, kiongozi huyo amekubali kukutana tarehe 5 mwezi ujao wa Desemba ikiwa utafanyika nchini Switzerland au Austria. Iwapo pande zote mbili zitakubaliana, hiyo itakuwa ni mara ya kwanza kwa Iran kukutana kujadili mpango wake wa nyuklia baada ya zaidi ya mwaka mmoja.
Wapatanishi wa nchi za Magharibi wanasema hawana tatizo na Iran kumiliki kiwanda cha nyuklia kwa matumizi ya kiraia, lakini wanataka hakikisho kwamba mpango huo hautumiwi kurutubisha kwa siri madini ya Uranium hadi kiwango cha kuweza kutengeneza silaha za nyuklia.
Mwandishi Maryam Abdalla/Rtre/Afpe
Mhariri:Prema Martin