Iran: Polisi waonya kuhusu 'maandamano ya kutumia silaha'
3 Januari 2026
Polisi nchini Iran imesema kuwa maandamano nchini humo yanazidi kusambaa na kuwa ya ghasia kubwa. Shirika la habari la Fars limemnukuu msemaji wa polisi akisema kuwa hawatoruhusu maadui wa nchi hiyo kugeuza maandamano ya amani kuwa machafuko na uasi wa kutumia silaha, na kwamba watalinda taifa na watu hadi pumzi ya mwisho.
Kile kilichoanza Tehran kama maandamano ya kupinga ugumu wa maisha na kupanda kwa mfumuko wa bei, kimegeuka kwa haraka kuwa machafuko ya kisiasa ya kitaifa yakiambatana na kaulimbiu dhidi ya uongozi wa taifa hilo la Kiislamu. Vyombo vya habari vya umma vimeripoti vifo vya watu 10 na watu 30 kukamatwa.
Kulingana na shirika la habari la Fars, vikundi vinavyodaiwa kupangwa kutoka nje ya nchi vimefanya mashambulizi dhidi ya majengo ya umma kote nchini.