1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran: Tunaweza kupunguza urani iliyorutubishwa kwa masharti

10 Februari 2026

Mkuu wa masuala ya nyuklia nchini humo amesema taifa hilo linaweza kukubali kupunguza viwango vya urutubishaji wa madini ya urani ili badala yake iondolewe vikwazo vyote vya kifedha ilivyowekewa.

Iran Teheran 2026 | Ayatollah Ali khamenei
Kiongozi mkuu wa Jamhuri ya Kiislam ya Iran, Ayatollah Ali KhameneiPicha: Office of the Iranian Supreme Leader/WANA/REUTERS

Wanadiplomasia wa Marekani na Iran walifanya mazungumzo kupitia wapatanishi wa Oman wiki iliyopita katika juhudi za kufufua mazungumzo kati yao baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuweka vikosi vyake vya kijeshi vya majini katika eneo hilo na kuzua hofu ya kufanyika kwa mashambulizi ya kijeshi siku chache zilizopita.

Mazungumzo hayo yanafuatia siku chache baada ya kuzimwa kwa maandamano ya kupinga serikali nchini Iran mwezi uliopita ambapo maelfu ya watu waliuawa na kupelekea machafuko makubwa zaidi ya ndani tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979.

Wakati wa maandamano hayo Rais Trump ambaye anataka Iran iachane na mipango yake ya kurutubisha Urani alitishia kwamba nchi yake ingeliingilia kati kijeshi lakini hatua hizo hazikufanyika.

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran,Mohammad Eslami, amesema hapo jana kwamba upo uwezekano wa kupunguza urani iliyorutubishwa kwa 60% lakini akaweka wazi kwamba hilo linategemea kama vikwazo walivyowekewea vitaondolewa au la.

Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Sipa USA/picture alliance

Eslami, ambaye matamshi yake yaliripotiwa na shirika la habari la ISNA la Iran, alisema hata hivyo kwamba pendekezo lingine, la kupeleka urani iliyorutubishwa ya Iran kwenda nchi nyingine, halijajadiliwa katika mazungumzo na maafisa wa Marekani.

Kwa upande wake kiongozi mkuu wa Jamhuri hiyo ya Kiislam, Ayatollah Ali Khameneiakizungumza hapo jana amesema kwamba bado taifa la Iran liko Imara licha ya juhudi mbalimbali za mataifa ya kigeni za kutaka kuvuruga hali nchini humo.

“Wakati mapinduzi ya 22 yalipotokea, taifa la Iran lilipata ushindi mkubwa. Liliweza kujiokoa katika kutoingiliwa na nchi za kigeni. Katika miaka hii yote, mataifa hayo ya kigeni yamekuwa yakitafuta kurejesha hali ya awali. Taifa la Iran limesimama imara.”amesema Khamenei.

Maafisa wa ngazi ya juu Iran ziarani Oman

Wakati hayo yakijiri,  Ali Larijani, mshauri wa karibu wa Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei  na katibu wa baraza lake la usalama wa taifa, wanaitembelea Oman hii kufuatia mazungumzo yao na Marekani na yaliyofanyika nchini humo, hayo ni kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim .

Ali Larijani, mshauri wa karibu wa Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali KhameneiPicha: Courtney Bonneau/SIPA/picture alliance

Katika ziara hiyo Larijani atakutana na maafisa wa ngazi za juu wa Usultani wa Oman na kujadili maendeleo ya hivi karibuni ya kikanda, kimataifa na ushirikiano wa pande mbili katika ngazi mbalimbali.

Iran na Marekani zilianza tena mazungumzo nchini Oman siku ya Ijumaa kwa mara ya kwanza tangu vita vya Iran na Israel vya siku 12 Juni mwaka jana,lakini tarehe kwa duru ya pili ya mazungumzo  bado hayajatangazwa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW