1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran: Tunaufunga tena Mlango Bahari wa Hormuz

18 Aprili 2026

Kamandi Kuu ya Jeshi la Iran imetangaza leo Jumamosi kurejesha vizuizi vyote kwenye Mlango Bahari wa Hormuz, hatua inayobadili msimamo wake iliyouchukua jana Ijumaa wa kuufungua ujia huo muhimu wa bahari.

Iran | Ghuba ya Uajemi
Mlango Bahari wa Hormuz ni ujia muhimu wa biashara ya mafuta na gesi duniani.Picha: Rouzbeh Fouladi/MEI/SIPA/picture alliance

Hapo jana Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran Abbas Araghchi alitangaza kufunguliwa kikamilifu wa Mlango Bahari wa Hormuz kama sehemu mazungumzo yake na Marekani.

Tehran iliifunga njia hiyo nyembamba ya bahari inayopitisha karibu asilimia 20 ya mafuta na gesi yote asili duniani baada ya Marekani na Israel kuishambulia dola hiyo ya Uajemi mwishoni mwa mwezi Februari.

Hii leo, taarifa iliyotolewa na Kamandi Kuu ya Jeshi la nchi hiyo imesema Washington imekiuka ahadi ya kufungua kikamilifu shughuli zote za usafirishaji kupitia mlango habari huo kwa uamuzi wake wa kuendelea na mzingiro wa kijeshi iliyouweka mwanzoni mwa wiki hii.

Rais Donald Trump wa Marekani aliamuru jeshi la nchi hiyo kuweka vizuizi kwa shughuli zote za bandari za Iran ikiwa ni pamoja na kuzuia kuingia na kutoka kwa meli zinazobeba shehena ya mafuta ya Iran.

Uamuzi huo aliuchukua kufuatia kukosekana kwa makubaliano baina ya pande hizo mbili zilipokutana kwa mazungumzo ya amani mjini Islamabad, Pakistan wikendi iliyopita.

Chini ya mzingiro huo wa Marekani, meli zote zilizokuwa zinaelekea au kutoka kwenye bandari na mwambao wa bahari ya Iran zimekuwa zikizuiwa na jeshi la wanamaji wa Marekani.

Tehran yasema Marekani imevunja uaminifu kwa kuendelea na mzingiro

Iran imesema hadi pale Marekani itakapoondoa mzingiro kwa meli zinazoelekea kwenye dola hiyo ya kiislamu, "hali kwenye Mlango Bahari wa Hormuz itasalia chini ya usimamizi mkali" wa Tehran.

Msemaji wa Kamandi Kuu ya Jeshi la Iran amesema hapo kabla Iran ilikubali "kwa nia njema" kuruhusu idadi kubwa ya meli za mafuta na biashara kukatiza Mlango Bahari wa Hormuz lakini "kwa bahati mbaya, Wamarekani wameendelea kuipaka tope imani iliyoanza kujengeka, na kujihusisha na vitendo vya uharamia na wizi baharini".

Tangazo la siku ya Ijumaa kutoka Iran la kuufungua Mlango Bahari wa Hormuz lilipokelewa kwa furaha kila kona ya dunia hasakutokana na msukosuko wa sekta ya nishati duniani ulioshuhudiwa tangu njia hiyo ilipofungwa na kuwa chini ya udhibiti wa Tehran.

Rais Trump aliikaribisha hatua hiyo kwa bashasha, lakini akasema mzingiro wa Washington dhidi ya meli za Iran utaendelea hadi pale pande hizo mbili zitakapofikia makubaliano ya mwisho.

Rais Donald Trump wa Marekani. Picha: CNP/ADM/Capital Pictures/picture alliance

Trump pia ametishia kurejea tena kwa mashambulizi dhidi ya Iran ikiwa hakuna mkataba utakaopatikana.

Akijibu swali na mwandishi habari usiku wa kuamkia leo Jumamosi, kuhusu nini atafanya iwapo hapatakuwa na makubaliano na Iran wakati muda wa usitishaji mapigano wa sasa utakapomalizika wiki ijayo, Trump alisema, "Sifahamu, pengine tutarefusha (usitishaji mapigano), lakini mzingiro utaendelea kuwepo. Lakini pengine naweza nisirefushe, kwa hiyo tutakuwa na mzingiro na pengine kwa bahati mbaya itabidi tuanze kuvurumisha tena mabomu."

Juhudi za kidiplomasia zinaendelea kuhakikisha pande hizo mbili zinarejea mezani haraka iwezekenavyo ili kuepusha kuanza tena kwa makabiliano ya kijeshi. Pakistan iliyokuwa mwenyeji wa mazungumzo ya kwanza inatazamiwa kuwa tena mwenyeji wa duru ya pili ambayo inaaminika itafanyika wiki ijayo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW