1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran: Tutalipa kisasi kwa mauaji ya Soleimani

4 Januari 2020

Iran imeendelea kutoa ahadi ya kulipa kisasi dhidi Marekani ambayo ilitekeleza shambulizi la anga lililomuua kamanda wa ngazi ya juu wa jeshi la nchi hiyo Qassem Soleimani.

Protest in Iran After US Airstrike Kills Iranian Commander
Picha: picture-alliance/dpa/R. Fouladi

Akitoa matamshi sawa na yaliyotolewa na viongozi wakuu wa Iran, balozi wa Iran kwenye Umoja wa mataifa amesema kifo cha Jenerali Soleimani ni sawa na kuanzisha vita na "jibu la hatua ya kijeshi hutolewa kwa njia za kijeshi".

Balozi Majid Takht Ravanchi amekiambia kituo cha televisheni cha CNN kuwa kuuliwa kwa kamanda huyo wa jeshi, Marekani imeingia kwenye awamu nyingine ya vita baada ya kuanzisha ´vita ya kiuchumi´ kwa kuiwekea Iran vikwazo vikali mwaka 2018.

Ravanchi amesema Iran itachukua hatua kali za kulipa kisasi na kwamba nchi yake tayari imeliarifu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa Tehran inayo haki ya kujilinda chini ya sheria ya kimataifa.

Katika barua yake kwa baraza hilo na kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ravanchi amesema mauaji ya Soleimani ni mfano wa wazi wa ugaidi na kitendo cha kihalifu kinachokiuka kwa kiwango cha juu misingi ya sheria ya kimataifa hususan mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Viongozi wa ulimwengu watoa wito wa utulivu 

Picha: Reuters/WANA/N. Tabatabaee

Wakati huo huo, viongozi wa mataifa mbalimbali wameonya jana kuwa shambulizi la Marekani lililomua kamanda wa ngazi ya juu wa jeshi la Iran limeongeza kitisho duniani na linaweza kuitumbukiza mashariki ya kati kwenye mzozo mkubwa wa kijeshi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kila upande kujizua dhidi ya kuongeza msuguano akisema ulimwengu hauko tayari kwa vita nyingine kwenye eneo la Ghuba.

Wito kama huo umetolewa pia na Urusi, Ujerumani, Ufaransa, Muungano wa Falme za Kiarabu, Syria na Saudia Arabia.

Hata hivyo Uingereza, Ujerumani na Canada ambazo ni washirka wa Marekani wamesema Iran inabeba jukumu kwa kile kilichotokea kutokana na tabia yake ya hivi karibuni ya uchokozi wa kijeshi

Katika hatua nyingine bei ya mafuta duniani imepanda jana Ijumaa baada ya Marekani kumuua kamanda wa ngazi ya juu wa jeshi la Iran, kisa kilichozusha hofu ya kuibuka mzozo kwenye kanda ya mashariki ya kati iliyo tajiri kwa mafuta.

Kufuatia kifo cha Jenerali Qasem Soleimani, bei za mafuta zimepanda kwa zaidi ya asilimia 3 kwenye soko la dunia wakati Iran ikionya kuchukua hatua nzito kulipa kisasi dhidi ya Marekani.

Marekani kuongeza idadi ya wanajeshi kwenye kanda hiyo

Picha: picture-alliance/dpa/Cpt. R. Haake

Mjini Washington maafisa wa wizara ya ulinzi, Pentagon, wamesema Marekani itapeleka wanajeshi 3000 wa ziada kwenye eneo la mashariki ya kati kukabiliana na kitisho kinachoongezeka.

Kadhalika Marekani imewatolea wito raia wake kuondoka haraka nchini Iran na kwamba ubalozi wake ulioshambuliwa na waandamanaji wanaounga mkono makundi ya kishia umefungwa na shughuli kaitka balozi ndogo zimesitishwa.

Katika kisa kingine saa 24 tangu shambulizi lililomua Soleimani kutokea, maafisa nchini Iraq na wanamgambo wa kishia wanaoungwa mkono na Iran wameripoti shambulizi jingine lililoyalenga magari mawili.

Afisa mmoja wa serikali ya Iraq amearifu kuwa shambulizi hilo limetokea kaskazini ya mji mkuu Baghdad lakini akaongeza kwamba hakuwa na taarifa za kutosha kuhusu madhara yaliyotokea.

Afisa mwingine wa usalama amesema watu watano wamekufa kwenye shambulizi hilo lililoulenga msafara wa matabibu wa kundi la wanamgambo wa kishia la  Popular Mobilization Forces.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW