Iran: Tutavishambulia vikosi vya Marekani vikiingia Hormuz
4 Mei 2026
"Tumerudia kusema kwamba usalama wa Mlango-Bahari wa Hormuz unadhibitiwa na vikosi vya jeshi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na katika mazingira yoyote, njia yoyote salama lazima iratibiwe na vikosi vya jeshi," alisema Meja Jenerali Ali Abdollahi , Kamanda wa Khatam al-Anbiya.
Ni taarifa ya meja Meja Jenerali Ali Abdollahi wa kamandi kuu ya jeshi la Iran ikisomwa kwenye kituo cha utangazaji cha IRIB. Abdollahi amesisitiza kwenye taarifa hiyo akivionya vikosi vyovyote vya kigeni na hususan jeshi vamizi la Marekani kwamba ikiwa watajaribu kuingia Mlango Bahari wa Hormuz watashambuliwa.
Marekani, leo Jumatatu imeanza rasmi utekelezaji wa juhudi zake za kulinda meli zilizokwama katika Mlango Bahari huo wa Hormuz, siku moja baada ya Rais Donald Trump kutangaza kile alichokiita "Project Freedom". Hata hivyo Trump hakutoa maelezo ya kina kuhusu namna operesheni hiyo itakavyofanyika, huku mapema leo, Idara ya Operesheni za Majini ya Umoja wa Falme za Kiarabu -UKMTO- ukiarifu kuhusu kushambuliwa kwa meli kwenye Mlango Bahari wa Hormuz.
Kulingana na idara hiyo, meli hiyo ilishambuliwa Jumapili jioni na makombora ambayo hayajulikana ikiwa njiani, kama kilomita 145 kaskazini mwa Fujairah, Umoja wa Falme za Kiarabu.
Kulingana na Kituo cha Pamoja cha Taarifa za Majini leo Jumatatu, Marekani ilikuwa imeanzisha "eneo lenye usalama ulioimarishwa” kusini mwa njia za kawaida za usafirishaji baharini na kuwahimiza mabaharia kushirikiana kwa karibu na mamlaka za Oman "kutokana na matarajio ya kuongezeka kwa idadi ya meli,” kwenye Mlango huo wa bahari ulioko kati ya maeneo ya Iran na Oman.
Huku hayo yakijiri, mapema jana Jumapili, Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, kimeiambia Marekani kwamba imesaliwa na machaguo mawili, ama kuanzisha operesheni ya kijeshi "isiyowezekana” au kufikia makubaliano na Tehran, baada ya Rais Trump kulipuuzilia mbali pendekezo jipya la amani la Iran.
Wizara ya mambo ya nje ya Iran ilisema mjini Tehran kwamba iliwasilisha mpango wenye vipengele 14 unaolenga kumaliza vita, na Washington tayari imejibu kupitia ujumbe uliowasilishwa kupitia mpatanishi, Pakistan, na ambao Iran ilikuwa ikiupitia.
Na huko Yerevan, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameitolea wito Marekani na Iran kuufungua tena Mlango Bahari wa Hormuz kwa uratibu wa mataifa yote mawili, wakati jeshi la Marekani likiendelea na operesheni hiyo ya kusindikiza meli.
Kwenye mkutano wa viongozi wa Ulaya huko Armenia, Macron amesema hilo ndiyo suluhisho pekee la kufungua tena Mlango-Bahari huo na kusisitiza kwamba hawatashiriki kwenye operesheni yoyote ya kijeshi ambayo mfumo wake hauko wazi. Ikumbukwe, Ufaransa na Uingereza walianzisha pia juhudi za kuunda muungano wa kuufungua upya mlango huo baada ya kufikiwa kwa makubaliano ya amani.