1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran, Urusi na Uturuki zakutana Astana juu ya Syria

16 Machi 2018

Mawaziri wa nje wa Urusi, Iran na Uturuki wanakutana nchini Kazakhstan kuzungumzia vita vinavyoendelea Syria, ambako majeshi ya nchi zao ni washiriki wa moja kwa moja yakiunga mkono pande tafauti.

Kasachstan Syriengespräche in Astana
Picha: picture-alliance/AA/C. Ozdel

Mazungumzo haya ya madola matatu yanayojihusisha moja kwa moja na vita vya Syria yanakuja ikiwa ni mwezi mmoja tu tangu utawala unaoungwa mkono na Urusi na Iran kuanza mashambulizi yake makali dhidi ya eneo linaloshikiliwa na upinzani la Ghouta Mashariki, kando kidogo ya mji mkuu, Damascus.

Hali mbaya ya kibinaadamu kwenye eneo hilo huenda ikawa moja ya ajenda za mazungumzo hayo, wakati Mohammad Javad Zarif wa Iran, Sergei Lavrov wa Urusi na Mevlut Cavusoglu wa Uturuki wakikutana mjini Astana hivi leo.

Akizungumza kandoni mwa mkutano huo, Lavrov alisema kuwa "mamilioni ya Wasyria wanaelekeza macho yao mjini Astana" wakati madola hayo makubwa yenye nguvu kwenye mzozo huo yakisaka njia za kuumaliza.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, Staffan de Mistura, hataweza kuhudhuria mkutano huo wa Astana, ingawa naibu wake, Ramzi Ramzi, atamuwakilisha.

Kazakhstan imekuwa mwenyeji wa duru kadhaa za mazungumzo juu ya Syria tangu Januari mwaka jana yanayoungwa mkono na mataifa hayo matatu, nyingi zao zikihudhuriwa pia na wawakilishi wa serikali na upinzani nchini Syria.

Mkutano huu unatazamiwa kuweka msingi wa mkutano wa kilele wa marais wa nchi hizo tatu unaopangwa kufanywa tarehe 14 Aprili mjini Istanbul, Uturuki.

Macho yote Ghouta Mashariki

Ingawa sehemu kubwa ya nchi imo kwenye mapambano, katika siku za karibuni, macho ya ulimwengu yameelekezwa zaidi kwenye eneo la Ghouta Mashariki, ambako takribani watu 1,200 wameshauawa tangu serikali ya Rais Bashar Al Assad kuanza operesheni yake ya mabomu na mizinga kujaribu kulitwaa kutoka mikononi mwa waasi katikati ya mwezi uliopita.

Raia wakikihama kitongoji cha Ghouta Mashariki yanakoendelea mashambulizi ya serikali dhidi ya ngome za waasi.Picha: Getty Images/AFP/L. Beshara

Vikosi vitiifu kwa Rais Assad vinaaminika kuwa sasa vinadhibiti zaidi ya asilimia 70 ya eneo hilo, ambalo kwa jana peke yake lilikimbiwa na raia 20,000, kwa mujibu wa Shirika la Uangalizi wa Haki za Binaadamu la Syria.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameielezea hali kwenye ngome hiyo kuu ya zamani ya waasi kuwa ni sawa na "jahanamu ya duniani", kukiwa na ukosefu mkubwa wa chakula, maji na huduma nyengine za msingi.

Uturuki, ambayo inawaunga mkono waasi, imetoa wito wa kuondolewa kwa mzingiro dhidi ya Ghouta Mashariki, ingawa yenyewe inaendelea kushambulia mji wa kaskazini mwa Syria, Afrin, ambao unadhibitiwa Wasyria wenye asili ya Kikurdi.

Makubaliano ya kutengwa maeneo manne yasiyoruhusika shughuli za kivita yaliyofikiwa mjini Astana mwaka jana, yalisifiwa kwa kupunguza uhasama kati ya serikali na waasi, lakini yalitajwa kuwa hayana maana na Marekani baada ya mashambulizi ya serikali kwenye eneo la Ghouta Mashariki kuanza mwezi uliopita.

Zaidi ya watu 340,000 wameuawa tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2011, ambavyo vimeigeuza jamhuri hiyo ya Kiarabu kuwa uwanja wa mataifa makubwa duniani kuoneshana ubabe.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW