1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran: Wabunge waidhinisha muswada wa sheria kali za mavazi

20 Septemba 2023

Wabunge nchini Iran wamepiga kura na kuidhinisha muswada wa kuongeza adhabu kwa wanawake wanaokiuka kanuni na maadili ya mavazi ya Kiislamu. Wanawake wanaweza kukabiliwa na adhabu ya kifungo cha hadi miaka 10 jela.

Iran | Frauen Kopftuch
Picha: Atta Kenare/AFP/Getty Images

Vyombo vya habari vya Iran ikiwa ni pamoja na shirika rasmi la habari la IRNA vimeripoti kuwa Bunge la nchi hiyo limeidhinisha kwa muda wa majaribio wa miaka mitatu, kile kilichotajwa kuwa " Muswada unaounga mkono utamaduni wa Hijabu na kujilinda na matendo yasiyokuwa halali". Hata hivyo muswada huo bado unahitaji kuidhinishwa na Baraza la katiba ambalo  lina  mamlaka makubwa nchini humo.

Tangu maandamano makubwa ya mwaka jana, wanawake nchini Iran wamekuwa wakizidi kukiuka kanuni kali za mavazi za Jamhuri hiyo ya Kiislamu, ambazo zinawataka wanawake kujihifadhi kwa kuvaa mavazi ya heshima na kufunga  hijabu.

Soma pia: Makundi ya Haki: Iran imezuia kumbukumbu ya kifo cha Mahsa

Maandamano hayo yalizuka baada ya kifo cha Mahsa Amini mwenye umri wa miaka 22, ambaye alikamatwa na Polisi wa maadili kwa madai ya kukiuka kanuni za mavazi. Mamia ya watu waliuawa, wakiwemo maafisa kadhaa wa usalama, huku maelfu ya wengine wakikamatwa kwa kile maafisa wa Tehran walisema  ni "machafuko" yaliyochochewa na mataifa ya kigeni.

Wanawake wakiandamana jijini London, Uingereza wakidhihirisha mshikamano kwa wanawake wa Iran: 13.09.2023Picha: Justin Ng/Avalon/picture alliance/Photoshot

Rasimu ya sheria hiyo inabaini kuwa, wanawake watakaokaidi kuvaa hijabu au mavazi yanayofaa, kwa ushirikiano na serikali za kigeni au vyombo vya habari, vikundi au mashirika yaliyotajwa kuwa maadui wa Iran, watakabiliwa na kifungo cha miaka 5 hadi 10 jela. Kwa wanawake, kufunika kichwa na shingo ni lazima nchini Iran tangu miaka ya 1979 baada ya  mapinduzi ya Kiislamu.

Raia wa Iran waandamana nje ya Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Takriban watu wapatao 100 wanaoupinga utawala wa Iran wameandamana hapo jana mjini New York kunakoendelea Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambapo miongoni mwa mambo mengine, wamelaani ukandamizaji dhidi ya wanawake. Kiongozi wa maandamano hayo Anahita Sami amesema:

" Iran ya leo, utawala unawabagua wanawake na umefanya hilo kuwa sheria. Sheria za ndoa ndizo zenye ubaguzi zaidi. Mwanaume anaweza kuoa hadi wanawake wanne kwa wakati mmoja, na mwanamke anahitaji ridhaa ya msimamizi wa kiume, iwe baba au babu yake mzaa baba ili tu aruhusiwe kuolewa. Hizi ni baadhi tu ya sheria kandamizi zinazowakabili wanawake nchini Iran hii leo "

Binti raia wa Iran akishiriki maandamano ya watu wanaunga mkono mavazi ya hijab, Tehran:12.07.2023Picha: Atta Kenare/AFP/Getty Images

Katika miezi ya hivi karibuni, mamlaka na polisi wa doria wamezidisha shinikizo dhidi ya wanawake na wafanyabiashara ambao wameshindwa kuzingatia kanuni za mavazi. Baadhi ya makampuni yamefungwa kwa sababu ya kutofuata sheria hiyo huku kamera za uchunguzi zikiwekwa katika maeneo mbalimbali ya umma ili kuchunguza na kufuatilia ukiukaji wa sheria ya mavazi.

(Chanzo: AFPE)

 

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW