1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaadhimisha siku ya Jerusalem kwa kuitishia Israel

Daniel Gakuba
29 Aprili 2022

Maelfu ya Wairan wameshiriki katika maandamano mjini Tehran Ijumaa, kuadhimisha siku ya Jerusalem ambayo Iran inasema ni tukio la kuelezea mshikamano na Wapalestina. Yalikuwa maandamano ya kwanza tangu janga la corona.

Iran Proteste von Arbeitern
Picha: ILNA

 

Iran imekuwa na utamaduni wa kuiadhimisha siku hiyo kila Ijumaa ya mwisho ya mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, tangu mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979, yaliyoongozwa na hayati Ayatollah Ruhollah Khomeini. Inajulikana rasmi kama siku ya Quds, neno Kiarabu kumaanisha Jerusalem.

Soma zaidi: Marekani, Israel zakutana na nchi za Kiarabu dhidi ya Iran

Waandamanaji walihanikiza sauti wakisema ''kifo kwa Israel,'' na ''kifo kwa Marekani,'' matamshi ambayo yamekuwa nembo ya maandamano nchini Iran tangu Mapinduzi ya Kiislamu. Vile vile bendera za Marekani, Uingereza na Israel huwa zinachomwa moto.

Baada ya maandamano hayo kituo cha televisheni ya taifa hilo kimeonyesha makombora ya aina mbli mbali ya masafa marefu, ikiyaelezea kama ''mishale ya kuipiga Israel.''

Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ndicho chenye nguvu zaidi nchini IranPicha: IRGC/WANA/REUTERS

Adui nambari moja wa Israel kikanda

Iran hailitambui taifa la Israel, badala yake inaunga mkono makundi ya Hezbollah na Hamas ambayo ni mahasimu wa Israel. Kwa upande wake, Israel huichukulia Iran kama adui yake nambari moja katik ukanda wa Mashariki ya Kati.

Maandamano ya leo ya mjini Tehran yameishia katika chuo kikuu cha mji huo mkuu, yakihitimishwa na sala ya Ijumaa adhuhuri. Miji mingine pia iliandaa shughuli kama hiyo.

Soma zaidi: Iran yasema haina nia ya kumiliki silaha za nyuklia

Shirika la habari la IRNA limemnukuu mwanajeshi mmoja wa cheo cha jenerali kutoka kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi, kijulikanacho kama jeshi la Quds, akisema kuwa Iran italiunga mkono kundi lolote lililo tayari kuipiga vita Israel.

''Tunaunga mkono mapambano yoyote ya kikosi kilichoundwa kwa ajili ya kupigana na uongozi wa kihalifu, na tuko tayari kushirikina na jumuiya yoyote iliyo tayari kuupiga vita uongozi huo dhalimu,'' amenukuliwa kusema Jenerali Esmail Ghaani katika mji wa Mashhad ulio kaskazini mashariki mwa Iran.

Rais wa Iran, Ebrahim RaisiPicha: WANA/REUTERS

Vigogo wa siasa za Iran washiriki

Viongozi wengi wa ngazi za juu wa Iran wamehudhuria maandamano ya mjini Tehran, ikiwa ni pamoja na Rais Ebrahim Raisi, na kamanda mwenye nguvu wa kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi, Jenerali Hossein Salami.

Soma zaidi:Mazungumzo ya nyuklia na Iran kuendelea Vienna

Akiwahutubia wandamanaji, Jenerali Salami ametoa onyo kwa Israel akisema majibu ya Iran ni ya uchungu, na kwamba Israel inatengeneza ''mazingira ya kujiangamiza yenyewe.'' Kamanda huyo ameendelea kuitisha Israel, akisema inajua kitakachoisibu ikiwa itajaribu kufanya ''matendo maovu.''

Israel imeapa kuishambulia kijeshi Iran, ikiwa mazungumzo baina ya nchi hiyo na mataifa yenye nguvu duniani yatashindwa kuzuia mchakato wa Iran wa kuunda silaha za nyuklia. Iran husisitiza kuwa mpango wake wa atomiki ni kwa ajili ya matumizi ya amani.

rtre, ape