1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaahidi kuchukua hatua sawa kwa Marekani

Grace Kabogo AFP, AP, Reuters
1 Septemba 2026

Rais wa Iran Masoud Pezeshkian, amesema nchi yake itachukua hatua sawa iwapo Marekani itarejea kutekeleza ahadi ilizotoa chini ya makubaliano ya muda ya mwezi Juni yaliyolenga kuvimaliza vita kati ya nchi hizo mbili.

Tehran, Iran 2026 | Rais wa Iran Masoud Pezeshkian
Iran imesisitiza ni muhimu kuhakikisha Rais Donald Trump anatekeleza ahadi zilizowekwa katika makubaliano yaliyosainiwaPicha: Iranian Presidency/UPI Photo/IMAGO

 Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amesema nchi yake itachukua hatua sawa iwapo Marekani itarejea kutekeleza ahadi ilizotoa chini ya makubaliano ya muda ya mwezi Juni yaliyolenga kuvimaliza vita kati ya nchi hizo mbili.

Pezeshkian ameitoa kauli hiyo Jumanne mjini Bishkek wakati akijiandaa kukutana na Rais wa Urusi, Vladimir Putin pembezoni mwa mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai, SCO.

Vita havina maslahi kwa pande zote

Pezeshkian amesema vita havina manufaa kwa upande wowote ule, na kwamba Iran bado imefungua mlango kwa kupatikana suluhisho la mazungumzo katika mzozo wake na Marekani.

Iran imerudia kusema kuwa itaruhusu meli kupita kwa uhuru katika Mlango Bahari wa Hormuz ambao umeendelea kuwa chanzo kikuu cha mvutano, ikiwa Marekani itatekeleza masharti ya makubaliano ya muda yaliyosainiwa kati ya Marekani na Iran mwezi Juni, kwa lengo la kumaliza uhasama kati yao ulioanza mwishoni mwa mwezi Februari kutokana na mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Mlango Bahari wa Hormuz umeendelea kuwa chanzo kikuu cha mvutanoPicha: REUTERS

Kulingana na Pezeshkian, Iran haitaki vita, lakini itajibu kwa nguvu na uthabiti dhidi ya uchokozi wowote ukaofanywa dhidi yake. Siku ya Jumatatu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi pia aliihimiza Marekani kurejea katika kutekeleza ahadi zake na yale ambayo Rais Donald Trump alisaini. Amesema kwa kuzingatia hali hiyo, kila kitu kinaweza kurejeshwa kwenye mkondo sahihi.

Aidha, Rais Trump ameonya kuwa ataishambulia vibaya Iran, baada ya mataifa hayo mawili kushambuliana tena kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja.

Mashambulizi yaanza tena

Mvutano huo uliongezeka baada ya Marekani kushambulia kwenye kisiwa cha Iran cha Larak, katika Mlango Bahari wa Hormuz siku ya Jumapili, na Iran kujibu kwa kuzishambulia kambi za kijeshi za Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amezitolea wito Iran na Marekani kujizuia kwa kiwango cha juu, baada ya nchi hizo mbili kurejea katika mapigano mwishoni mwa juma lililopita.

Umoja wa Mataifa wataka mazungumzo ya kidiplomasiaPicha: Yiannis Kourtoglou/REUTERS

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, amesema hali ya kurejea kwa mapigano hayo inasikitisha kwa sababu kulikuwa na takribani mwezi mmoja wa angalau utulivu wa muda.

''Kwa mara nyingine tena, Katibu Mkuu anatoa wito kwa pande zote kurejea katika mazungumzo ya kidiplomasia, yatakayosaidia kupatikana kwa suluhisho na hivyo kurejesha utulivu na kuimarisha imani katika ukanda huo," alisisitiza Dujarric.

Iran yakanusha madai kuhusu uchumi wake 

Katika hatua nyingine Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Bessent amekutana na Mawaziri wa Fedha wa kundi la nchi tajiri na zinazoinukia kiuchumi za G20, wakati ambapo Marekani ikizishinikiza nchi nyingine kusaidia kuitenga Iran kiuchumi, huku vita vya Iran na mivutano ya kibiashara vikiendelea kuathiri uchumi wa dunia na kusababisha kupanda kwa bei ya mafuta.

Hata hivyo, Gavana wa Benki Kuu ya Iran, Abdolnaser Hemmati amesema Jumanne kuwa nchi hiyo ina akiba ya kutosha ya fedha za kigeni licha ya vikwazo vya Marekani. Hemmati amepinga madai ya Marekani kwamba uchumi wa Iran umedhoofishwa kiasi cha kuilazimisha nchi hiyo kuchukua hatua za kijeshi au za kulipiza kisasi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW