1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaandaa uchaguzi wake wa kwanza wa bunge tangu 2022

2 Machi 2024

Iran inafanya uchaguzi wa kwanza wa bunge, tangu maandamano makubwa ya kupinga serikali. Uchaguzi huo unaonekana kama mtihani kwa uhalali wa uongozi wa taifa hilo wakati kukiwa na malalamiko juu ya kushuka kwa uchumi

Iran | Uchaguzi
Kiongozi wa kidini nchini Iran Ayatollah Ali KhameneiPicha: picture alliance/dpa

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa mapema leo Ijumaa, ili kuwachagua wanachama wa bunge na bodi ya viongozi wa kidini, huku kukiwa na ghofu ya idadi ndogo ya watu kushiriki uchaguzi huo, ambao wahafidhina wanatarajiwa kuendelea kubakia madarakani.

Kiongozi wa kidini nchini Iran Ayatollah Ali Khamenei, aliouita mchakato huo wa uchaguzi kama wajibu wa kidini, alikuwa wa kwanza kupiga kura katika kituo cha Imam Khomeini Hussainia.

Iran yajiandaa kwa uchaguzi unaohodhiwa na wahafidhina

Khamenei amesema, macho ya marafiki na maadui wa Iran yapo katika matokeo ya uchaguzi huo wa bunge, akitoa wito wa kuwafurahisha marafiki wa Iran na kuwakasirisha maadui wa taifa hilo la kiislamu.

Shirika la habari la Iran limekuwa likionyesha vidio za watu wanaoimba nyimbo za kizalendo huku wengine wakionekana wamepanga mistari mirefu tayari kwa kupiga kura zao.

Baadhi ya wapiga kura wasema wamejitokeza kumfurahisha Khamenei

Idadi ndogo ya wapiga kura yaripotiwa katika uchaguzi wa bunge IranPicha: Vahid Salemi/picture alliance/AP Photo

Mpiga kura mmoja aliliambia shirika hilo kwamba yeye amepiga kura ili kumfurahisha kiongozi wa kidini nchini humo. Zaidi ya wagombea 15,000 wanapigania viti vya bunge 290. Matokeo ya mwanzo kabisa yanatarajiwa kutolewa kesho Jumamosi.

Licha ya haya kuarifiwa wanaharakati na makundi ya upinzani yameendeleza # ya VOTENoVote na # ElectionCircus katika mtandao wa kijamii wa X uliojulikana kama Twitter zamani, zote zikihimiza kutopiga kura katika uchaguzi waliouita wa mchezo wakisema watu wakijitokeza kwa wingi hiyo itakuwa ni kama kuhalalisha utawala katika Jamhuri hiyo ya kiislamu.

Iran yafanya uchaguzi wa kwanza wa bunge tangu kifo cha Mahsa Amini

Walioshuhudia wanasema vituo vingi vya kupigia kura havikuwa na watu mjini Tehran na miji mingine mingi. Mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel aliyefungwa jela nchini humo Narges Mohammadi, ambaye ni mwanaharakati wa kutetea haki za wanawake ameuelezea uchaguzi huo kama mzaha.

Wanaharakati wasema uchaguzi ni wa mzaha

Uchaguzi huo ni kwanza tangu kufanyika maandamano ya kupinga serikali mwaka 2022 na 2023 yaliyosababisha mgogoro mkubwa wa kisiasa kuwahi kuonekana tangu mapinduzi ya mwaka 1979.

Mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel na mwanaharakati wa kutetea haki za wanawake Iran Narges MohammadiPicha: DW

Watawala wa Iran bila shaka wanataka watu wengi kujitokeza kushiriki uchaguzi huo ili kutakasa uwepo wao ambao umechafuliwa vibaya na maandmano yaliyoitikisa nchi hiyo.

Lakini kulingana na uchunguzi uliofanyika ni asilimia 41 pekee ya wairan waliojisajili kupiga kura.

Mwaka 2020 asilimia 42.5 ya wapiga kura walijitokeza kushiriki uchaguzi wa bunge, ikilinganishwa na mwaka 2016 ambapo asilimia 62 walishiriki.

Vyanzo: reuters/afp

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW