Iran yaigeukia China katika harakati za kuviepuka vikwazo
17 Januari 2025Jumuiya ya Kimataifa inafuatilia kwa karibu hatua zinazopigwa na Iran katika mipango yake ya nyuklia, wakati kundi la mataifa matatu ya Uingereza, Ufaransa na Ujerumani ama E3 yakielezea utayari wa kukitumia kipengele chenye nguvu cha kidiplomasia kilichopo kwenye mpango wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa, ikiwa Tehran itaendelea kuzalisha silaha za nyuklia.
"Snapback" ni kipengele cha kidiplomasia, ambacho ni sehemu ya ya makubaliano ya mkataba unaoyumba wa nyuklia wa Oktoba 2015 ama JCPOA. Chini ya mkataba huo, mataifa yaliyotia saini yalikubaliana kuiondolea vikwazo Iran, ili nayo iachane na mipango yake ya nyuklia, ambavyo kwa kiasi kikubwa viliudhoofisha uchumi wa taifa hilo.
Kuna nini kwenye Mkataba nyuklia wa JCPOA?
Mkataba wa JCPOA unairuhusu Iran kutekeleza mipango yake ya nyuklia, lakini kwa malengo ya kibiashara, tiba na kiviwanda na kwa kuzingatia viwango vilivyokubalika vya kimataifa vya kuzuia kuenea kwa silaha za maangamizi.
Hata hivyo, makubaliano hayo yalitupiliwa mbali wakati wa utawala wa Rais aliyepita wa Marekani Donald Trump, aliyeiondoa Marekani na kuvirejesha vikwazo, katika awamu ya kwanza ya utawala wake, mwaka 2018.
Soma pia:Trump: 'Hatutathibitisha makubaliano ya nyuklia na Iran'
Na mwezi Disemba, 2024, mataifa hayo matatu ya Uingereza, Ufaransa na Ujerumani yaliishutumu Iran kwa kuongeza hifadhi ya madini ya urani "yaliyorubutibishwa kwa viwango vya juu kabisa".
Hatua hii ilichukuliwa baada ya shirika la kimataifa la Umoja wa Mataifa la kudhibiti Nguvu za Atomiki, IAEA kusema kwamba Iran ilikuwa ikirutubisha madini hayo kwa hadi asilimia 60, ikielekea asilimia 90, kiwango ambacho huhitajika ili kutengeneza silaha.
Snapback itamaanisha nini kwa Tehran?
Ikiwa kipengele cha "snapback" kitatumiwa, vikwazo vyote vilivyowekwa dhidi ya Iran kwenye makubaliano hayo ya mwaka 2015 vitarejeshwa na kulifanya taifa hilo kukabiliwa na kitisho kikubwa cha anguko la uchumi.
Mkakati wa Iran wa kuepuka hali kama hiyo umejikita katika kuimarisha ushirikiano wake wa kimkakati, na China, kama mjumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na mwenye jukumu muhimu katika kutegua kitendawili cha mivutano ya kimaeneo kwenye baraza hilo.
Soma pia:Iran yasema iko tayari kutatua masuala yenye utata kuhusu nyuklia
Hata hivyo, chaguo la kipengele hicho linafikia ukomo wake mwezi Oktoba mwaka huu, hali inayoongeza udharura wa juhudi za kidiplomasia ambazo zimekuwa zikiendelea kati ya Iran na mataifa hayo ya E3.
Nafasi ya China na ukomo wa uungaji wake mkono kwa Iran
Wakati mvutano ukiongezeka kati ya Iran na mataifa ya Magharibi, taifa hilo sasa limeigeukia China kama mshirika katika kukabiliana na hali hiyo.
China kwa muda mrefu imekuwa na ushirika wa kibiashara na Iran na ushirika huo umeendelea kuimarika na hasa kwenye sekta ya nishati. Hivi karibuni wakati Waziri wa Mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi, anayeongoza taifa hilo kwenye mazungumzo kuhusu masuala ya nyuklia, alielezea matumaini yake kwenye gazeti la People's Daily ya kufunguka kwa ukurasa mpya wa kimahusiano baina ya mataifa hayo.
Soma pia:China, Iran watoa mwito wa kuondolewa vikwazo vya Iran
Hata hivyo, uungaji mkono wa China kwa Iran unasalia kuwa tete kuliko Iran inavyoamini. Wakati Beijing wakati wote ikiitetea Iran dhidi ya vikwazo vya Magharibi, lakini kubadilika kwake katika vipaumbele vya kimataifa kunalifanya taifa hilo kuitekelza mbinu yake hiyo kwa tahadhari.
Utegemezi wa China kwenye mafuta ghafi kutoka Iran, unaofanya asilimia 13 ya bidhaa inazoingiza kutoka nchini humo kunaashiria umuhimu wa Iran katika sera ya nishati ya China.
Lakini, kurejea kwa Donald Trump pamoja na matarajiao kwamba huenda akarejesha "sera yake ya shinikizo la juu" kwa Iran ni dhahiri kwamba uhusiano huu unaweza kukabiliwa na changamoto kubwa. Utekelezwaji mkali wa vikwazo, unaweza kuvuruga uingizwaji wa mafuta ghafi na ya bei ya chini huko China, hatua itakayoongeza gharama kwenye sekta ya kusafisha mafuta na kuathiri uchumi.
Soma pia:Vikwazo vyaathiri biashara ya bidhaa za kiutu Iran
Iran inavyopambana kupata uungwaji mkono wa China
Katikati ya kitisho kwamba kipengele cha "Snapback" kinaweza kurejesha vikwazo vikali, ushawishi wa Iran kwa China unazidi kupungua.
Licha ya uungaji mkono wa jumla wa China kwa mamlaka ya Iran, malengo mapana ya Beijing ya kisiasa na kiuchumi yanazidi nia yake ya kuiependelea moja kwa moja Iran. Hii inajumuisha na namna China inavyotanguliza uhusiano na madola yenye nguvu na mataifa ya Ghuba ya Uajemi.