1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaanza kuwazuia wakaguzi ya nyuklia

23 Februari 2021

Serikali ya Iran imetangaza rasmi kuanza kwake hatua ya kuzuia ukaguzi wa wataalamu wa kimataifa katika vinu vyake vya shughuli za nyuklia. Hatua hiyo ikiwa ni utekelezaji wa sheria mpya ya taifa hilo ambayo imeanza leo

Iran - Atomabkommen | IAEA-Generaldirektor Rafael Grossi reist nach Teheran
Picha: Lisi Niesner/REUTERS

Hatua hiyo ambayo imetangazwa kupitia televisheni ya umma wa taifa hilo inatajwa kuwa na lengo la kuzishinikiza nchi za Umoja wa Ulaya pamoja na utawala mpya wa Marekani chini ya Rais Joe Biden kuiondolea nchi hiyo vikwazo vya kiuchumi pamoja na kuurejesha tena mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015, ambao ulipoteza nguvu zake baada ya Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump kujichukulia mamlaka binafsi ya kuliondoa taifa lake katika makubaliano hayo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya televisheni ambayo haikutoa maelezo ya kina, inaleta tafsiri ya moja kwa moja kwamba Iran imetoa kitisho hicho kwa nia ya kupunguza kiwango cha ushirikiano na waangalizi wa Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Nguvu za Atomiki, IAEA. Hatua ni utelezaji wa sheria mpya taifa hilo ambayo imeanza leo hii (23.02.2021) ambayo iliridhiwa na bunge la taifa hilo miezi kadhaa iliyopita.

Wakaguzi wa IAEA hawapata vidio mubashara

Kinu cha nyuklia cha katika moja ya eneo la IranPicha: SalamPix/abaca/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif amesema shirika hilo halitopata uwezekano wa kuona vidio za moja kwa moja kutoka katika maeneo ya vinu vya nyuklia badala yake linapewa zilizorekodiwa.

Baada ya  kuanza kwa utekezaji wa sheria hiyo, shirika la taifa la nguvu za atomiki la Iran, limetoa ahadi ya kutunza mikanda ya vidio kwa miezi mitatu, na kisha itaikabidhi kwa shirika la IAEA, lakini kwa masharti ya kupata unafuu wa vikwazo ilivyowekewa. Lakini pia imetishia kwamba itaweza kuifuta mikanda hiyo ya vidio endapo kutakuwa na dirisha finyu la upatikanaji wa suluhu ya kidemorasia.

Hatua ya Iran ya kutangaza kusitisha utekelezaji wa kile kilichoitwa itifaki ya ziada, ikiwa ni makubaliano ya siri kati ya Iran na IAEA, ilifikiwa kama sehemu ya mkataba wa kihistoria wa nyuklia wa Iran. Makubaliano hayo yalikuwa yanatoa fursa ya wakaguzi wa Umoja wa Mataifa kutoka IAEA kuwa na nguvu ya kuvitembelea vinu vya nyuklia na kukagua mpango wa nyuklia wa Iran.

Lakini karibu miaka mitatu iliyopita, rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, aliiondoa Marekani katika mpango huo wa Iran na kuiwekea vikwazo vya kiuchumi nchi hiyo, jambo ambalo limeliathiri taifa hilo hadi wakati huu.

Chanzo: APE