1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya awali ya nyuklia ya Iran yaanza Uswisi

28 Novemba 2021

Timu ya wajumbe wa Iran kwenye mazungumzo ya nyuklia imekutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya wawakilishi wa mataifa yaliyosaini Mkataba wa Nyuklia wa mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa yenye nguvu ulimwenguni.

Iran | Videostill | Anlage zu Uran-Anreicherung in Natanz
Picha: IRIB/AP Photo/picture alliance

Shirika la habari la Iran (ISNA) limeripoti kwamba timu hiyo inayoongozwa na Ali Bagheri Kani ilifanya mazungumzo ya awali na wawakilishi wa mataifa hayo kuelekea mazungumzo ya Jumatatu (Novemba 29).

"Kikosi cha Iran kiliwasili Vienna siku ya Jumamosi (Novemba 27) na kikaanza mikutano ambayo iliendelea hadi Jumapili katika kiwango cha wataalamu na wakuu wa timu za Urusi na China na pia mratibu wa Umoja wa Ulaya, Enrique Mora," mwanadiplomasia wa Iran, Mohammadreza Ghaebi aliliambia shirika la habari la ISNA.

Marekani chini ya Biden inashiriki kwa mara ya kwanza.

Rais Joe Biden wa MarekaniPicha: Evan Vucci/AP/picture alliance

Marekani, ambayo chini ya rais wa sasa Joe Biden, inashiriki kwa mara ya kwanza mazungumzo hayo na Iran siku ya Jumatatu katika njia isiyo ya moja kwa moja, inaarifiwa kutokuwa na matumaini madogo ya kuunusuru Mkataba wa Nyuklia ya Iran wa mwaka 2015 na uwezo wake mdogo wa kuizuwia Tehran kutengeneza bomu la nyuklia ikiwa mazungumzo haya yatashindwa.

Tangu aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump, kuiondowa nchi yake kwenye Mkataba huo mwaka 2018 na kurejesha vikwazo dhidi ya Iran, ambavyo vilikuwa vimeondoshwa na masharti ya Mkataba wenyewe, Iran nayo iliamua kukiuka masharti kadhaa yaliyowekwa kwa mpango wake wa nyuklia.

Serikali ya Marekani imeonesha nia ya kutaka kurejea katika mkataba wa 2015 wa nyuklia.

Biden amesema anataka kurejea kwenye mkataba huo - uliowekwa saini mwaka 2015 chini ya Rais Barack Obama wakati yeye Biden akiwa makamu wake - endapo tu Iran itarejea kwenye masharti ya awali.

Mazungumzo hayo yasiyo ya moja kwa moja mjini Vienna yanakuja baada ya zuio la miezi mitano lililowekwa na Iran, na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alisema siku ya Jumatano kwamba "ipo nafasi ya kufikia makubaliano haraka na kutekeleza yaliyoafikiwa."

Lakini mjumbe maalum wa Marekani kwa Iran, Rob Malley, amesema kwamba "tabia ya Iran haiendani vyema na mazungumzo."

Mara kadhaa, Marekani imekuwa ikiilaumu Iran kwa mwendo wa kowa na kuongeza matakwa mapya kila mara, huku wakati huo huo ikifanya jitihada zinazoweza hatimaye kuifanya iwe na bomu la nyuklia.

Kwa upande wake, Iran imekanusha mara zote kuwa na mpango wa kuunda silaha za kiatomiki na badala yake inasema teknolojia yake ya nyuklia ni kwa ajili ya matumizi salama ya nishati na matibabu, kama inavyotumiwa na mataifa mengine kadhaa ulimwenguni.

Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri: Sudi Mnette