1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran italipiza kisasi dhidi ya walioushambulia ubalozi wake

Angela Mdungu
2 Aprili 2024

Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesema nchi yake italipiza kisasi dhidi ya shambulio linalodaiwa kufanywa na Israel katika ubalozi mdogo wa Tehran kwenye mji mkuu wa Syria, Damascus.

Raisi wa Iran akizungumza katika moja ya mikutano ya srikali Tehran
Rais wa Iran Ebrahim RaisiPicha: Iranian Presidency via ZUMA Press/picture alliance

Kauli hiyo imetolewa siku moja baada ya makamanda kadhaa wa jeshi la Iran kuuawa katika tukio hilo

Raisi, amelielezea shambulio hilo dhidi ya ubalozi wake mdogo mjini Damascus kuwa ni uhalifu wa kigaidi. Ameongeza pia kuwa kitendo hicho ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na kutahadharisha kwamba uhalifu huo hautopita bila kuwaadhibu waliohusika.

Kwenye shambulio hilo, majenerali wawili na maafisa wengine watano wa jeshi la walinzi wa mapinduzi la Iran waliuwawa. 

Waliouwawa watambuliwa.

Iran imewatambua majenerali waliouwawa kuwa ni Mohammad Reza Sahedi na msaidizi wake Mohammad Hadi Haji.  Shirika la habari la Iran  la Tasnim limeripoti kuwa, Sahedi ndiye aliyekuwa akiongoza operesheni nchini Syria na Lebanon. Licha ya shutuma za Iran, serikali ya Israel haijatoa tamko lolote kuhusu tuhuma hizo.

Soma zaidi: Wapiganaji 9 na kamanda wauwawa kwa mashambulizi Syria

Kulingana na waziri wa mambo ya kigeni wa Iran, Hossein Amirabdollahian kupitia jukwaa la X, Iran imemuita mwakilishi wa kidiplomasia wa Uswisi na kumpa ujumbe muhimu wa kidiplomasia kwa Marekani kuhusu shambulio hilo la Jumatatu. Hata hivyo hapakutolewa taarifa zaidi kuhusu ujumbe huo.

Itakumbukwa kuwa Uswisi imekuwa ikiwakilisha maslahi ya Marekani kwa Tehran tangu uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili ulipovunjika miaka 24 iliyopita.

Eneo lililolengwa na mashambulizi ya anga mjini Damkaribu na ubalozi wa Iran mjini DamascusPicha: MAHER AL MOUNES/AFP

Mashambulizi hayo yanayodaiwa kufanywa na Israel dhidi ya ubalozi wa Tehran nchini Syria yamefanyika sambamba na kampeni inayoendelea dhidi ya kundi la Hamas linaloungwa mkono na Iran.

China yalaani mashambulizi yaliyoulenga ubalozi wa Iran mjini Damascus

Katika hatua nyingine, China imeyalaani mashambulizi ya anga yanayodaiwa kufanywa na Israel yaliyouharibu ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus. Msemaji wa wizara ya ulinzi ya China Wang Wenbin amesema, usalama wa taasisi za kidiplomasia haupaswi kukiukwa.

Ameongeza kuwa, uhuru na uadilifu wa kieneo nchini Syria vinapaswa kuheshimiwa. Wenbin amesema hali ya sasa ya mashariki ya kati ni mbaya na wanapinga vitendo vyovyote vitakavyosababisha mivutano iongezeke.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW