Iran kukubaliana na Marekani katika kubadilishana wafungwa
12 Machi 2023Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amirabdollahian amesema wamefikia makubaliano ya kubadilishana wafungwa na Marekani na kwamba yapo matumaini hatua hiyo itatekelezwa mapema.
Kupitia televisheni ya umma ya taifa hilo waziri huyo amesema kwa upande wa Iran kila kitu kipo tayari lakini kwa upande wa Marekani wapo katika masuala ya mwisho ya kiufundi.
Vyanzo vya taarifa nchini Iran vililiambia shirika la habari Reuters kuwa nchi mbili hizo zimekuwa katika mfululizo wa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kwa kufanikisha lengo la kuwaachia huru wafungwa.
Mmoja kati ya Wamarekani walio kizuizini Iran ni Siamak Namazi, mfanyabiashara mwenye uraia pacha wa Marekani na Iran, ambaye mwaka 2016 alihukumiwa miaka 10 gerezani kwa kosa la upelelezi na kushirikiana na serikali ya Marekani.