1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaendelewa kubanwa kuhakikisha haina mpango wa kutengeneza silaha za kinyuklia

31 Oktoba 2003

Leo ndiyo siku ya mwisho kwa Iran kutoa kauli ya mwisho kuhusu mpango wake wa nyuklia na kuthibitisha kwamba haina mpango wa kutengeneza silaha za kinyuklia, kama ilivyoagizwa na taasis ya kimataifa ya nishati ya nyuklia IAEA. Mkurugenzi wa taasis hii, Mohamed ElBaradei, amesema, mpaka sasa Iran imetoa nyaraka nyingi kukidhi matakwa hayo, lakini taasisi yake inahitaji muda wa kuzifanyia kazi nyaraka hizo, kabla ya kusema imeridhika au la.

Wataalamu wa Taasis ya kimataifa ya nishati ya kinyuklia IAEA hivi sasa wanaendelea kukagua nyaraka za Iran na maeneo kadhaa nchini humo. Taasisi hii iliyo na makao yake makuu mjini Viena-Austria imesema, itatoa ripoti kamili hapo tarehe 20-Novemba, ripoti ambayo itaambatana na uamuzi, kama suala hili litapelekwa kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa au la. Kiongozi wa taasisi hii, Mohamed ElBaradei amenukuliwa akisema, mpaka sasa anaridhika na hatua waliyofikia kwenye ukaguzi wanaofanya. Itakumbukwa kuwa, Iran ilikuwa imepewa muda maalumu kutoa maelezo yote ya mpango wake wa atomu hadi kufikia mwisho wa mwezi wa Oktoba, yaani leo hii, na hapohahapo ilitakiwa kusaini makubaliano mengine ya ziada ya kupinga kusambaza silaha za kinyuklia na hapohapo kusitisha mpango wa kuandaa madini ya urani ambayo yanaweza kutumiwa katika utengenezaji wa silaha za kinyuklia.

Wiki moja kabla ya siku ya mwisho kufika, hapo tarehe 23-Oktoba, Iran iliikabidhi taasisi husika nyaraka nyingi za kurasa 200 hivi na kudai kwamba, nyaraka hizo zina majibu ya maswali yao yote. Lakini hatua hii ilifikiwa na Iran baada ya mawaziri wa nchi za nje wa Ujerumani, Uingereza na Ufaransa kuitembelea nchi hiyo na kuishawishi kuafiki mambo mawili ya msingi kabisa: Kwanza, kwamba Iran inasitisha shughuli zote za kuandaa madini ya Uran ambayo yanaweza kutumiwa kutengenezea silaha za kinyuklia. Na pili Iran inasaini mikataba ya nyongeza ya kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia. Mikataba hii ya nyongeza inamaanisha kwamba, Iran itakuwa tayari kukaguliwa kikamilifu saa yeyote ile na taasisi husika.

Lakini siku chache baada ya maafikiano hayo, Iran iliendelea kutoa maelezo ya kutatanisha, kiasi cha wahusika wakaanza kutilia shaka msimamo wa Iran. Mathalan: Jumapili tarehe 26-Oktoba, msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Iran, Asefi, alisema, mpango wa kuandaa madini ya Uran kwa ajili ya kutengenezea hata silaha, tayari umeshasitishwa. Muda mfupi baadaye, wizara hiyohiyo ikatoa taarifa kwamba, msemaji wa wizara amekosea, hatua ya kusitisha maandalizi ya madini ya Uran ndiyo kwanza inafanyiwa kazi. Naye kiongozi wa mpango wa atomu nchini humo, Ayatollah Rowhani alinukuliwa akisema, Iran haisitisha kamwe mpango wake wa kuandaa madini ya Uran. Licha ya utata huo, serikali ya Iran bado haijapitisha makubaliano ya ziada ya kuzuia kuenea kwa silaha za atomu, ikidai kwamba, makubaliano hayo lazima upitishwe bungeni kwanza.

Hata hivyo wadadisi wa mambo wanaona Iran imefikia hatua nzuri kwa kuwaruhusu wakaguzi wa taasis husika kuingia nchini humo na kuanza shughuli za ukaguzi. Mpaka sasa wamekuwa wakikagua mabaki ya madini ya Uran ambayo tayari wameyakuta kwenye mashine fulani. Marekani imesema, huo ni uthibitisho wa kutosha kwamba Iran ilikuwa ina mpango wa siri wa kutengeneza silaha za atomu. Hata hivyo Iran imekanusha tuhuma hizo kwa madai kwamba, mashine hizo zilinunuliwa kwenye masoko ya magendo katika nchi za nje katika miaka ya 80 zikiwa na mabaki hayo ya Uran.

Taasis ya kimataifa ya nishati ya nyuklia imesema takribani nchi 40 duniani hivi sasa zina uwezo wa kutengeneza silaha za kinyuklia. Hili ni tishio kubwa kwa ulimwengu na ndiyo maana taasisi hii inadai mkataba wa kuzuia kuenea kwa silaha za kinyuklia udurusiwe upya. El Baradei alipokuwa akiongea na waandishi wa habari nchini Ufaransa alisema, mkataba huu ambao ulianza kufanya kazi mnamo mwaka 1970 umepitwa na wakati -- utengenezaji wa silaha za nyuklia unazivutia nchi nyingi pamoja na vikundi vya kigaidi. Licha ya hivyo wataalamu wa mambo wanasema, hivi sasa silaha za nyuklia zinaweza kutengenezwa katika muda wa miezi kadhaa tu. Kwa hiyo wahusika wa mambo wametoa wito wa kupitia upya mkataba huu, zaidi ya marekebisho machache yaliyofanywa mwaka 1995 mara baada ya vita vya kwanza vya Ghuba.


Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW