1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaikamata meli ya Israel licha ya onyo la Biden

13 Aprili 2024

Licha ya onyo la Rais Joe Biden wa Marekani kwa Iran kutokuishambulia Israel, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran limeikamata meli moja linayosema ina "uhusiano na utawala wa Kizayuni" kwenye Ghuba ya Uajemi.

Meli karibu na Mlango Bahari wa Hormuz
Helikopta ya jeshi la Iran kwenye operesheni ya kuikamata meli inayohusishwa na Israel karibu na Mlango Bahari wa Hormuz siku ya Jumamosi (Aprili 13).Picha: picture alliance/AP

"Meli ya makoneta iitwayo 'MCS Aries' imekamatwa na Kikosi Maalum cha Jeshi la Majini cha Sepah baada ya operesheni ya anga", liliripoti shirika la habari la Iran (IRNA) siku ya Jumamosi (Aprili 13).

IRNA ilisema kuwa operesheni hiyo ilifanyika "karibu na Mlango Bahari wa Hormuz" na kwamba "meli hiyo saa imepelekwa kwenye eneo la mamlaka ya Iran.

Soma zaidi: Biden aitahadharisha Iran kutoishambulia Israel

Masaa machache baada ya kusambaa kwa taarifa ya kushikiliwa kwa meli hiyo, msemaji wa jeshi la Israel alisema Iran ingelibeba lawama endapo machafuko yangelisambaa kwenye eneo la Mashariki ya Kati.

"Iran itaona matokeo ya kuchaguwa kuifanya hali kuzidi kuwa mbaya," alisema Daniel Hagari kwenye taarifa yake, akiongeza kwamba Israel ilikuwa kwenye hali ya juu ya hadhari.

"Tumeongeza utayari wetu wa kuilinda Israel dhidi ya uchokozi zaidi wa Iran. Pia tuko tayari kujibu mashambulizi." Alisema.

'MCS Aries inamilikiwa na Zodiac Maritime, kampuni ya meli ya kimataifa ambayo miongoni mwa wamiliki wake ni mfanyabiashara wa Kiisraeli, Eyal Ofer.

Onyo la Biden

Haya yalijiri ikiwa ni siku moja tu baada ya Rais Biden kusema alikuwa anatazamia Iran ingeishambulia Israel "hivi karibuni" na kuionya Tehran dhidi ya kuchukuwa hatua hiyo.

Rais Joe Biden wa Marekani akiionya Iran dhidi ya kuishambulia Israel kulipiza kisasi kwa mauaji ya majenerali wake.Picha: DW

Alipoulizwa juu na waandishi wa habari juu ya ujumbe wake kwa Iran siku ya Ijumaa (Aprili 12), Biden alisema kwa ufupi: "Usiishambulie", huku akitilia mkazo ahadi ya Washington kuilinda Israel.

Soma zaidi: Uingereza yashuku kuvamiwa kwa meli mlango bahari wa Hormuz

"Tumejitolea kwenye ulinzi wa Israel. Tutaiunga mkono Israel. Tutasaidia kuilinda Israel na Iran haitafanikiwa," alisema rais huyo wa Marekani.

Biden alisema asingelifafanuwa zaidi taarifa za siri, lakini alisema matazamio yake ni kuwa mashambulizi hayo ya Iran yangelifanyika "muda wowote kutoka sasa."

Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari akiwa kwenye Ikulu ya White House baada ya hotuba ya hotuba yake kwenye kongamano la haki za kiraia.

Siku ya Ijumaa, gazeti la Wall Street Journal liliripoti kuwa Marekani ilipeleka meli zake pamoja na vikosi vya kijeshi kwenye ukanda wa Mashariki ya Kati kwa ajili ya kuilinda Israel, ikitarajia kuyatenguwa mashambulizi yoyote ya moja kwa moja kutoka Iran dhidi ya Israel, ambayo yalikhofiwa yangelifanyika ama Ijumaa au Jumamosi.

Hatua hiyo ya Marekani, ambayo inadai ni sehemu ya juhudi za kuepusha mgogoro mkubwa zaidi kwenye eneo hilo ilikuja baada ya onyo kutoka kwa mtu mmoja aliyetajwa kuwa na uelewa wa mambo hayo juu ya wakati na mahala ambapo mashambulizi ya Iran yangelifanyika, kwa mujibu wa jarida hilo.

Hata hivyo, mtu mwengine aliyedai kupewa taarifa na uongozi wa Iran, alisema ingawa mipango ya mashambulizi ilikuwa inajadiliwa, kulikuwa hakujafikiwa maamuzi rasmi, liliripoti gazeti hilo.

Raia wa kigeni waombwa kuondoka

Mataifa kadhaa, zikiwemo India, Ufaransa, Poland na Urusi zimewaonya raia wake kutokutembelea eneo hilo, ambalo tayari limekuwa kwenye ukingo wa vita katika Ukanda wa Gaza kwa mwezi wa saba sasa.

Mashambulizi ya Aprili 1, 2024 yaliyouwa maafisa wa kijeshi wa Iran kwenye ubalozi wake mjini Damascus, Syria.Picha: Firas Makdesi/REUTERS

Siku ya Ijumaa, Ujerumani iliwataka raia wake walioko nchini Iran kuondoka.

Soma zaidi: Israel katika hali ya tahadhari kufuatia kitisho cha Iran

Mapema, msemaji wa Ikulu ya Marekani, John Kirby, alisema mashambulizi ya Iran dhidi ya Israel ni kitisho cha kweli na kinachowezekana, ingawa hakueleza ni muda gani yangelifanyika.

Kirby alisema Marekani ilikuwa inavitegemea vikosi vyake kwenye eneo hilo endapo kungelifanyika mashambulizi hayo na kwamba walikuwa wanaifuatilia hali kwa ukaribu.

Siku ya Ijumaa, Israel ilikuwa kwenye hali ya hadhari ikikhofia mashambulizi kutoka Iran au kwa washirika wa taifa hilo la Ghuba ya Uajemi. 

Miito ya kulipiza kisasi

Kote kwenye ukanda huo, kumekuwa na miito ya kulipiza kisasi kutokana mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus, Syria, wiki iliyopita. 

Sala ya jeneza kwa maafisa wa kijeshi wa Iran waliouawa kwa mashambulizi dhidi ya ubalozi wa nchi hiyo mjini Damascus, Syria, tarehe 1 Aprili 2024.Picha: AP/picture alliance

Mashambulizi hayo, ambayo Iran na Marekani zinaamini yalifanywa na Israel, yaliwauwa watu wanane, miongoni mwao akiwamo kamanda ngazi za juu wa Kikosi Maalum cha Walinzi wa Mapinduzi wa Iran anayesimamia vikosi vya nje vya Quds.

Soma zaidi: Ufaransa yawarai raia wake kutozuru Mashariki ya Kati

Kama ambavyo imekuwa ikifanya kwenye mashambulizi mengine huko nyuma, kwenye mashambulizi haya ya Aprili Mosi, Israel pia haikusema kuwa ilihusika wala kukanusha.

Viongozi wa juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akiwamo Kiongozi Mkuu Ayatullah Ali Khamenei, walisema Israel "lazima iadhibiwe na itaadhibiwa" kwa mashambulizi hayo ambayo alisema yalikuwa sawa na kuishambulia Iran.

Sources: AFP, dpa, Reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW