1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaikamata meli ya mafuta huku wasi wasi ukiongezeka

Sekione Kitojo
18 Julai 2019

Majeshi ya ulinzi wa mapinduzi ya Iran yamekamata meli ya mafuta katika eneo la ghuba na kuwatia mbaroni wafanyakazi wake 12, wakiwashutumu kusafirisha mafuta kwa njia haramu, shirika la habari la Iran Tasnim limeripoti.

Iranisches Patrouillenboot vor Öltanker in Straße von Hormus
Picha: AFP/A.Kenare

Meli  hiyo ilikuwa  imebena  lita  milioni  moja za  mafuta  wakati  ilipokamatwa wakati  ikipita  katika  ujia  wa  maji  wa  Hormuz , kwa  mujibu  wa  shirika  la habari  la  Tasnim, ambalo  halikusema  ni  taifa  gani  meli  hiyo  inatoka ama inatoa  huduma  kwa  kampuni  gani. Eneo  hilo  la  ghuba  ni  moja  kati  ya maeneo  muhimu  ya  njia  ya  majini  kwa  ajili  ya  kusafirisha  mafuta. Iran imesema  meli  iliyokamatwa  ni  ile  ambayo  ilivutwa  na  kuondolewa  katika eneo  la  bahari  siku  ya  Jumapili baada  ya  meli  hiyo  kutuma  ujumbe  wa kuwapo  na  matatizo.

Meli ya mafuta ya Japan ikiwa katika katika kisiwa cha Fujairah nchini Emirati, meli hiyo ilishambuliwa wiki iliyopita.Picha: AFP/M. Khatib

Maafisa  wa  marekani  walisema  jana  kuwa  hawana  hakika  iwapo  meli  ya mafuta  iliyokuwa  ikiondolewa  kwa  kuvutwa  na  kuingia  katika  eneo  la maji  la  Iran  imekamatwa  ama  kuokolewa. Uingereza  imeiomba  Iran kutuliza  hali  ya  wasi  wasi  katika  eneo  la  ghuba, wakati  wakiahidi  kulinda maslahi  ya  meli zake  katika  eneo  hilo.

Eneo  hilo  limekuwa eneo  tete  wakati  hali  ya  wasi wasi  ikiendelea kuongezeka  kati  ya  Iran  na  Marekani  kuhusiana  na  kuvunjika  kwa makubaliano  ya  nyuklia  ya  Iran  na  mataifa  yenye  nguvu  duniani na  hofu inaongezeka kuwa  pande  hizo  mbili  zinasogea  karibu  na  makabiliano  ya kijeshi.

Shutuma za Marekani kwa Iran

Ujia  wa  maji au  mlango  bahari  wa  Hormuz hivi  karibuni  umekuwa  eneo la  matukio  kadhaa  yanayohusu meli  za  kibiashara.

Mapema mwezi huu  Uingereza  iliikamata  meli  ya  mafuta  ya  Iran  nje  ya eneo  mla  Gibraltar. Siku  kadhaa  baadaye  Uingereza  iliishutumu  Tehran kwa  kujaribu  kuzuwia  njia  ya  meli  moja  ya  mafuta  ya  Uingereza katika ujia  huo  wa  maji.

Ndege isiyo na rubani ya Marekani. Hivi karibuni Iran ilidungua ndege kama hiyo ikiwa katika eneo la mlango bahari la HormuzPicha: picture-alliance/US Air Force/Zumapress

Marekani  imeishutumu  Tehran  wa  kuhusika  na  mashambulizi  kadhaa dhidi  ya  meli  za  kibiashara  karibu na  ujia  huo  wa  maji.

Tangu  rais  Donald Trump  kuingia  madarakani  mwaka  2017, Marekani imeelekeza  nguvu  zake  katika  kampeni ya  kuiwekea  mbinyo  mkubwa Iran , ikiwa  ni  pamoja  na  kujitoa  kutoka  katika  makubaliano  ya  kinyuklia na  mataifa  yenye  nguvu duniani  na  Iran  mwaka  2015.

Mwezi  uliopita  Trump  alisema  alifikia  karibu  na  kuamuru mashambulizi  ya anga kwa  kulipiza  kisasi  dhidi  ya  Iran  kuiangusha  ndege  ya  Marekani  ya ujasusi  isiyokuwa  na  rubani karibu  na  ujia  huo.

Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/J. Ernst

Wizara  ya  ulinzi  hivi  karibuni  imesema  itaweka  vikosi  zaidi  na  meli katika  eneo  hilo  katika  juhudi  za  kuimarisha uchunguzi  wa  shughuli  za Iran.

Rais  wa  Urusi Vladmir Putin  na  rais  wa  Ufaransa  Emmanuel Macron wamejadili  kuhusu makubaliano  ya  kinyuklia  na  Iran  pamoja  na  mzozo wa mashariki  mwa  Ukraine , imesema  ikulu  ya  Urusi  Kremlin leo. Ufaransa inajaribu  kupunguza  wasi wasi  baada  ya  marekani kujitoa  kutoka makubaliano  hayo  ya  kinyuklia  mwaka  jana.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW