Iran yaikosoa Saudia kuhusu Yemen
18 Aprili 2015Tangu mwezi Marchi ushirika unaongozwa na Saudia umekuwa ukishambulia maeneo ya waasi wakishia wa jamiin ya wahouthi pamoja na wapiganaji wao washirika wanaomtii rais aliyeondolewa madarakani nchini Yemen Ali Abdulla Saleh.Iran inawaunga mkono waasi hao wakihouthi lakini inakanusha kwamba inawapa silaha au usaidizi wowote wa kijeshi.
Rais Rouhani akihutubia gwaride la kijeshi mjini Tehran katika hotuba ambayo ilirushwa moja kwa moja kupitia televisheni amesema kuwaua raia nchini Yemen hakutoiletea nguvu wala sifa Saudi Arabia. Kwa upande mwingine Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameitaja kampeini ya mashambulizi ya anga ya Saudi Arabia na washirika wake nchini Yemen kuwa ni mauaji ya halaiki na uhalifu mkubwa.
Iran imewasilisha mpango wake maalum wa kumaliza mgogoro huo unaozingatia mambo manne ambayo ni pamoja na kutolewa msaada wa kibinadamu,kuwepo mdahalo pamoja na kuundwa serikali itakayojumuisha pande zote ya umoja wa Kitaifa nchini Yemen baada ya pendekezo la kusitisha vita kukataliwa na Saudi Arabia.
Sambamba na hayo Rouhani ameishutumu Saudi Arabia kwa kuwapa silaha na kuyafadhili makundi ya kigaidi katika eneo la Mashariki ya Kati ikiwemo kwenye nchi za Syria,Lebanon na Iraq.Ikumbukwe kwamba Iran inamuunga mkono rais wa Syria Bashar al Assan pamoja na serikali ya Iraq katika mapambano dhidi ya makundi ya kisunni ya itikadi kali ikiwemo lile la Dola la Kiislamu IS.
Iran inasema kwamba Saudi Arabia na serikali za nchi nyingi za Mashariki ya Kati zinaunga mkono kundi hilo la dola la kiislamu.Wadadisi wa mambo wanahisi kwamba Saudi Arabia imeingia kwenye mtego hatari nchini Yemen na huenda ikajikuta imekwama na kutoka itakuwa kazi kubwa.
Pamoja na hayo China kwa upande mwingine imeitaka Saudi Arabia kuongeza juhudi za kutafuta suluhisho la kisiasa katika mgogoro huo.Rais wa China Xi Jinping amempigia simu Jumamosi(18.04.15) mfalme Salman wa Saudi kwamba hali ya Yemen inatia wasiwasi kwa wanachama wote wa baraza la usalama na hata kwa hali jumla ya usalama katika mashariki ya kati,na zaidi eneo la Ghuba,hivyo basi mchakato wa kupatikana azimio la kisiasa katika mgogoro huo unabidi uharakishwe.
China ambayo inachukua nafasi ndogo katika suala la diplomasia kwenye eneo la mashariki ya kati licha ya kwamba nchi hiyo inategemea kiasi kikubwa cha mafuta ya eneo hilo,imeshawahi huko nyuma kuzungumzia juu ya wasiwasi wake kuhusu ghasia zinazoendelea Yemen na kutoa mwito wa kupatikana suluhisho la kisiasa.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Mohammed Dahman