Iran yaingia enzi mpya ya uongozi huku vita ikizidi kuenea
9 Machi 2026
Iran imemtaja Mojtaba Khamenei, mwana wa kiongozi mkuu aliyeuawa, kuwa mtawala mpya wa Jamhuri ya Kiislamu na hivyo kumweka mamlakani kiongozi mwenye msimamo mkali wa kidini wakati vita hivyo vinavyozidi kuenea kanda ya Mashariki ya Kati vikisababisha bei za mafuta kupanda maradufu.
Katika kuadhimisha uteuzi wa kiongozi mpya, Iran imezindua mashambulizi mapya dhidi ya miundombinu ya nishati ya nchi za Ghuba na kuelekea pia Israel. Tel Aviv tayari imemtaja Mojtaba kuwa mtu atakayelengwa.
Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vimeripoti kwamba Baraza la Wataalamu ambalo ni chombo cha juu cha viongozi wa kidini mjini Tehran halikusita kumchagua kiongozi mpya licha ya ‘ukandamizaji wa kinyama wa Marekani na utawala mwovu wa Kizayuni'. Kisha vilionyesha kombora ambalo lililokuwa tayari kufyatuliwa likiwa na maandishi: ‘Kwa amri yako, Sayyid Mojtaba.
Kulingana na Balozi wa zamani wa Israel nchini Marekani Michael Oren wakati akizungumza na kituo cha utangazaji cha ABC News, kiongozi yeyote mpya wa Iran ambaye ataendeleza misimamo mikali huenda akalengwa na Israel.
Ameeleza kuwa: "Kwangu mimi inaonekana kwamba kiongozi yeyote anayekuja na kusema, ‘nitaendeleza kampeni ya kuharibu nchi hii,' basi Israel ina wajibu wa kujaribu kumuondoa. Lakini kama kungekuwa na kiongozi tofauti ambaye atasema, ‘Sikiliza, ninataka kubadilisha jinsi Iran inavyowasiliana na majirani zake, jinsi inavyoitazama dunia na jukumu tunaloliona Iran ikicheza katika kanda na kimataifa,' basi Israel isingekuwa na tatizo naye."
Iran yaendelea kuzilenga nchi za Ghuba
Wakati vita hivyo vikiingia siku yake ya 10, Iran imezishambulia nchi za ukanda wa Ghuba kwa makombora na ndege za droni ambapo Saudi Arabia ilizuia ndege zisizo na rubani zilizolenga visima vyake vya mafuta, huku kampuni ya nishati ya taifa ya Bahrain ikionya kwamba huenda isiweze kutimiza mikataba ya mauzo ya nje baada ya shambulio la kombora. Umoja wa Falme za Kiarabu na Kuwait nazo pia zimeripoti mashambulizi.
Baada ya mashambulizi dhidi ya kituo kikubwa cha mafuta cha Al Ma'ameer nchini Bahrain, ambayo yamesababisha moto na uharibifu wa mali, kampuni ya taifa ya nishati ya nchi hiyo, Bapco, ilijiunga na nchi jirani za Qatar na Kuwait kutoa tahadhari kwamba matukio yaliyo nje ya uwezo wake huenda yakasababisha kushindwa kutimiza malengo ya mauzo ya nje. Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Qatar ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, ametoa wito wa kupunguza mvutano katika vita vya Marekani-Israel dhidi ya Iran.
Bei za mafuta zapanda maradufu
Na bei za mafuta duniani zimeendelea kupanda kwa kasi ambapo bei ya pipa la mafuta ghafi imepaa na kuvuka dola 100 kwa mara ya kwanza tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine miaka minne iliyopita. Masoko ya hisa duniani ikiwemo yale ya Japan na Korea Kusini yametikisika huku madereva nchini Ufilipino wakionekana kupanga foleni kubwa kujaza magari yao mafuta na Vietnam ilijiandaa kuondoa ushuru wa uagizaji wa mafuta.
Rais Donald Trump amepuuzilia mbali kupanda kwa bei ya mafuta, suala ambalo ni nyeti kisiasa nchini Marekani akisema ni athari ndogo ya matokeo ya kuondoa kile alichokitaja kuwa kitisho kikubwa cha mpango wa nyuklia wa Iran.
Hayo yakiendelea, huko Lebanon nako mapigano yameongezeka. Wanamgambo wa Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran wamesema kuwa walikuwa wanakabiliana na wanajeshi wa Israel waliotua mashariki mwa Lebanon kwa helikopta 15 kutokea upande wa mpaka wa Syria. Lebanon ilitumbukia katika mzozo huo wiki iliyopita baada ya Hezbollah kuishambulia Israel kufuatia kuuawa kwa Khamenei mkubwa.