1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIran

Iran yaionya Marekani baada ya kuzamishwa kwa meli yake

5 Machi 2026

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amelaani hatua ya Marekani kuizamisha meli ya kivita ya nchi hiyo akilitaja hatua hiyo kama "ukatili baharini" na kuongeza kwamba Marekani "itajutia kwa uchungu" hatua hiyo.

Geneva | Umoja wa Mataifa | Waziri wa Mambo ya nje wa Iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi Picha: Jean Marc Ferré/MAXPPP/picture alliance

Ving'ora vya tahadhari vimesikika katika miji ya Tel Aviv na Jerusalem huku televisheni ya taifa ya Iran ikiripoti kwamba mashambulizi zaidi yalilenga pia vituo vya kijeshi vya Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi, amelishtumu Jeshi la Wanamaji la Marekani kwa kile alichokiita kufanya "ukatili baharini" kwa kuizamisha meli ya kivita ya Iran, IRIS Dena, katika Bahari ya Hindi, tukio lililosababisha vifo vya mabaharia 87 wa Iran. Araghchi amesisitiza kwamba hatua ya kuzamisha meli ya Iran ni kitendo cha uchokozi ambacho hakitapita bila majibu.

Mwanadiplomasia huyo ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii, "Kumbukeni maneno yangu, Marekani itakuja kujutia kwa uchungu kitendo hiki walichokifanya."

Na katika hatua isiyo ya kawaida, mmoja wa viongozi wa kidini nchini Iran Ayatollah Abdollah Javadi Amoli, ametumia hotuba aliyoitoa kupitia televisheni ya taifa kutoa wito wa kulipiza kisasi dhidi ya Israel na Rais wa Marekani Donald Trump.

"Piganeni na Marekani dhalimu, damu ya Trump iko mabegani mwangu," alisema katika kauli za nadra kutoka kwa Ayatollah – cheo cha juu miongoni mwa viongozi wa kidini wa madhehebu ya Shia.

Bunge la Marekani kupiga kura kuhusu azimio la kusitisha mashambulizi

Na huko Marekani kwenyewe, bunge linajiandaa kupiga kura leo kuhusu azimio la mamlaka ya vita ili kusitisha mashambulizi ya jeshi la nchi hiyo dhidi ya Iran - ishara ya wasiwasi ndani ya bunge kuhusu kuongezeka kwa kasi kwa mzozo huo unaoonekana kubadilisha vipaumbele vya Marekani.

Kura hiyo inakuja katika kipindi ambacho mvutano wa kimataifa unaongezeka na mjadala kuhusu mamlaka ya rais kuanzisha vita bila idhini ya bunge.

Hawa ni baadhi ya Wamarekani. "Hili sio jambo tunalopaswa kujiingiza. Marekani haina sababu yoyote ya kuwepo huko."

"Unajua, hakuna mtu anayesema "Kifo kwa Ufaransa au Uingereza.' Wanasema ‘Kifo kwa Marekani!' Mtu anaposema hivyo, ni tishio, na hali hiyo inapotokea, tunapaswa kusimama pamoja na kushikamana."

Uharibifu wa jengo mjini Tehran kufuatia mashambulizi ya anga ya MarekaniPicha: Fatemeh Bahrami/Anadolu/picture alliance

Hii itakuwa kura ya pili kufanyika kuhusu suala hilo ndani ya muda mfupi, baada ya Seneti kukataa azimio kama hilo, hatua iliyoweka wazi mgawanyiko kati ya Warepublican na Wademokrat.

Tofauti ya idadi ya kura za Ndio na Hapana katika baraza la wawakilishi inatarajiwa kuwa ndogo, huku matokeo yakitarajiwa kutoa taswira kuhusu kiwango cha uungwaji mkono au upinzani dhidi ya operesheni ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Iran pamoja na hatua ya Trump kulipita bunge ambalo ndio lenye mamlaka ya kutangaza vita.

Wakati hayo yakijiri, Umoja wa Ulaya EU na Baraza la Ushirikiano wa Nchi za Ghuba GCC wametoa wito wa kupunguza mvutano unaoendelea kupitia njia ya mazungumzo na diplomasia.

Katika taarifa yao ya pamoja, EU na GCC wamesema wanahofia kasi ya kuongezeka kwa machafuko na athari zake kwa usalama wa eneo hilo na dunia kwa ujumla. Wamesisitiza kwamba njia pekee ya kuzuia mgogoro mkubwa zaidi ni mazungumzo ya moja kwa moja, diplomasia ya kina, na kuheshimu sheria za kimataifa.

Mawaziri wa mambo ya nje wa pande hizo mbili wamesema wanatambua haki ya nchi za Ghuba kujilinda dhidi ya vitisho vinavyotoka Iran.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW