1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaitaka Marekani iondoe vikwazo dhidi yake

Zainab Aziz Mhariri:Saumu Njama
7 Februari 2021

Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameihimiza Marekani kuiondolea vikwazo vyote nchi yake iwapo Marekani inaitaka Iran izingatie makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa kati yake na nchi zenye nguvu ulimwenguni.

Iran | Ali Khamener tifft Mitgliedern des Nationalen Anti-Corona-Stab
Picha: MEHR

Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei alisema kwenye televisheni ya taifa kwamba Marekani inapaswa kuondoa vikwazo vyake dhidi ya Iran kabla ya nchi hiyo kuanza tena kufuata makubaliano yaliyofikiwa kati yake na nchi zenye nguvu ulimwenguni. Khamenei mwenye umri wa miaka 81, ndiye kiongozi mwenye uamuzi wa mwisho juu ya mambo yote ya serikali nchini Iran na ndiye aliyedhinisha juhudi za kufikia makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015.

Soma zaidi:Mataifa kadha yajaribu kuunusuru mkataba wa nyuklia na Iran

Rais aliyeondoka Donald Trump aliiondoa Marekani kwenye makubaliano hayo mnamo mwaka 2018. Kwa upande wake Iran ilijibu kampeni hiyo ya Trump ya kuishinikiza nchi hiyo kwa kukiuka polepole makubaliano ya nyuklia na ilisema kwamba itaongeza shughuli zake za kurutubisha madini ya Uranium kwa nia ya kumfanya rais mpya wa Marekani Joe Biden alipe kipaumbele swala hilo na kuirudisha Marekani kwenye makubaliano ya awali.

Mpaka sasa rais Biden ameshasaini hatua kadhaa kubadilisha amri zilizowekwa na mtangulizi wake yakiwemo pamoja na makubaliano ya mabadiliko ya hali ya hewa na swala la uhamiaji. Rais Biden ameonesha utayarifu wa nchi yake kuanzisha upya mazungumzo ya nyuklia na Iran kwa masharti kwamba Iran itasitisha hatua ilizochukua za kuongeza kurutubisha madini ya Uranium.

Kufuatia mauaji ya mwanasayansi wa Iran mnamo mwezi Desemba mwaka uliyopita, bunge la Iran liliidhinisha sheria ya kuwazuia wakaguzi wa kimataifa wa nyuklia kuingia nchini humo jambo ambalo linachukuliwa kuwa ni ukiukaji mkubwa wa makubaliano yaliyofikiwa.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Yemen Martin GriffithsPicha: Getty Images/AFP/M. Huwais

Hata hivyo Iran imesema hatua zake hizo zinazokiuka mkataba wa mwaka 2015 zinaweza kurekebishwa kwa urahisi iwapo pande zinazohusika zitazingatia mahitaji ya nchi hiyo na imesisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni kwa ajili ya matumizi ya kiraia.

Wakati huo huo mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Yemen Martin Griffiths ameanza leo ziara ya siku mbili nchini Iran. Ziara hiyo ni miongoni mwa hatua za kidiplomasia za kuunga mkono mpango wa amani nchini Yemen. Mjumbe huyo maalum wa Umoja wa mataifa atakutana na waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif na maafisa wengine wa nchi hiyo.

Soma zaidi:Iran kurutubisha madini ya Uranium kwa asilimia 20

Yemen imekuwa katika vita vya kugombea madaraka tangu mwishoni mwa mwaka 2014 kati ya serikali ya Yemen inayoungwa mkono na Saudia Arabia na waasi wa Houthi wanaohusishwa na Iran ambao wanaudhibiti mji mkuu wa Sanaa na maeneo mengine nchini Yemen. Ziara ya Griffiths ni sehemu ya juhudi zake za kidiplomasia zinazolenga kusaidia kupatikana suluhisho la kisiasa katika mzozo wa Yemen ambao utakidhi matarajio ya watu wa Yemen.

Ofisi ya mjumbe huyo maalum wa Umoja wa mataifa imesema kipaumbele cha ziara ya Griffiths ni kuunga mkono makubaliano kati ya wahusika kwenye mzozo huo na kufikia hatua ya kusitisha mapigano haraka ili shughuli za kusafirisha misaada ziweze kuanza tena pamoja na mchakato wa kisiasa. Mgogoro wa Yemen umeitumbukiza nchi hiyo kwenye umasikini mkubwa, baa la njaa na uharibifu miundombinu.

Vyanzo:/DPA/AP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW