1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yajibu pendekezo la usitishwaji mapigano

Bakari Ubena (dpa, ap, afp, reuters)
6 Aprili 2026

Iran imejibu pendekezo la usitishwaji mapigano na kufunguliwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz na kuelezea msimamo wake na kusisitiza kuwa mazungumzo "hayaendani na masharti wala vitisho vya kutenda uhalifu wa kivita.

Teheran | Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran Esmaeil Baghaei
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran Esmaeil Baghaei akijiandaa kuzungumza na waandishi wa habari mjini Tehran, IranPicha: Sha Dati/Xinhua/IMAGO

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran Esmaeil Baghaei amesema siku ya Jumatatu kuwa Tehran inazingatia matakwa yake kulingana na maslahi ya kitaifa ambayo tayari yamewasilishwa kupitia wapatanishi, na kuongeza kuwa matakwa ya awali ya Marekani kama vile mpango wenye vipengee 15 yamekataliwa kwa kuwa yalikuwa na "masharti kupita kiasi."

"Iran haina hofu kuelezea waziwazi kile inachokiona kama madai yake halali na kufanya hivyo hakupaswi kutafsiriwa kama ishara ya maelewano, bali kama kielelezo cha imani yake katika kutetea misimamo yake," alisema Baghaei katika mkutano na waandishi wa habari.

Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran ameendelea: " Tumeandaa majibu yetu wenyewe na tutatoa maelezo zaidi muda muafaka, aliongeza akijibu swali la mwandishi wa habari wa Iran kuhusu juhudi zinazoendelea za kusitisha mapigano kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Marekani na Iran, zilipokea rasimu ya pendekezo la usitishwaji mapigano kwa siku 45 pamoja na kufunguliwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz. Shirika la habari la AP, limesema pendekezo hilo liliwasilishwa na wapatanishi kutoka Misri, Pakistan na Uturuki na lilitumwa usiku wa Jumapili kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, pamoja na mjumbe maalum wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, Steve Witkoff.

Iran: Hatutoufungua Mlango-Bahari wa Hormuz

Mlago-Bahari wa Hormuz uliofungwa na IranPicha: Modis Team/Nasa Gsfc/ZUMA/IMAGO

Afisa mmoja wa Iran ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa nchi hiyo haitoufungua Mlango-Bahari wa Hormuz kama sehemu ya makubaliano ya usitishwaji mapigano na wala haitokubali kuwekewa muda maalum wa kulipitia pendekezo hilo.

Ripoti hiyo ya mpango wa usitishwaji mapigano inajiri baada ya Rais wa Marekani Donald Trump, kutoa muda wa mwisho wa siku ya Jumanne (07.04.2026) kwa Iran kuifungua njia hiyo muhimu ya baharini au miundombinu yake ya nishati ishambuliwe vibaya.

Bei ya mafuta imepanda kote duniani kutokana na vita vya Mashariki ya Kati na kufuatia hatua ya Iran kuufunga Mlango-Bahari wa Hormuz ambao unatumiwa kwa usafirishaji wa asilimia 20 ya mafuta na gesi yanayotumiwa kote ulimwenguni.

Mashambulizi: 25 wauawa Iran na 2 Israel

Aliyekuwa Mkuu wa ujasusi wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, IRGC, Meja Jenerali Majid Khademi ambaye aliuawa Jumatatu.Picha: Iranian Supreme Leader's Office/ZUMA/picture alliance

Zaidi ya watu 25 wameuawa nchini Iran kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel huku Jamhuri hiyo ya kiislamu, ikijibu kwa kuvurumisha makombora dhidi ya vituo vya Israel na Marekani katika mataifa jirani ya Ghuba.

Miongoni mwa waliouwawa katika mashambulizi ya Jumatatu ni mkuu wa ujasusi wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, IRGC, Meja Jenerali Majid Khademi. Israel kupitia waziri wake wa ulinzi Israel Katz imetangaza pia mauaji ya Khademi na ikasema itaendelea na mashambulizi yake ikiwalenga viongozi wa utawala iliyouita wa kigaidi.

"Kama tulivyosema awali: Ikiwa mashambulizi ya makombora dhidi ya raia wa Israel yataendelea, Iran italipia gharama kubwa. Tutashambulia na kusambaratisha miundombinu yake ya nishati na uwezo wa kushambulia wa utawala huo wa kigaidi. Kwa pamoja tutaendelea kuwalenga viongozi hao magaidi na kushambulia maeneo ya kiusalama na ya kimkakati kote Iran, ” alisema Waziri Katz.

Iran imeiushambulia pia mji wa Haifa nchini Israel na kuwaua watu wawili ambao walipatikana chini ya vifusi vya jengo lililoporomoka. Waokoaji wanaendelea na shughuli ya kutafuta miili pamoja na manusura.

Tehran yaonya kuhusu hatari ya janga la nyuklia

Mtu akiendesha baiskeli karibu na kinu cha nyuklia cha Iran cha BushehrPicha: Mehr News Agency/AP Photo/picture alliance

Shirika la kimataifa la kudhibiti matumizi ya nyuklia, IAEA, limethibitisha siku ya Jumatatu kuhusu athari za hivi karibuni za mashambulizi ya kijeshi karibu na kinu cha nyuklia cha Iran cha Bushehr, lakini likasema kiwanda chenyewe hakikuharibiwa.

IAEA imesema uthibitisho huo umetokana na uhakiki wake huru wa picha mpya za setilaiti na ufahamu wa kina wa eneo hilo, na kwamba shambulio moja lilipiga takriban mita 75 pekee kutoka kwenye eneo la kituo hicho. Wiki iliyopita shirika hilo lilisema liliarifiwa na Iran kuhusu shambulio la kombora karibu na eneo hilo.

Tehran imeikosoa siku ya Jumatatu IAEA kwa maneno makali kwa kile iliyosema ni kutochukua hatua baada ya  mashambulizi ya mara kwa mara ya Marekani na Israel karibu na kinu hicho pekee cha nyuklia cha Iran.

Katika barua kwa Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafael Grossi, mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran Mohammad Eslami alimkosoa kwa kushindwa kulaani vikali shambulio la hivi karibuni karibu na kiwanda cha nyuklia cha Bushehr, na kusisitiza kuwa hali hii ya kutokemewa inaweza kuchochea "wavamizi" kurudia mashambulizi kama hayo.

EU: Ni "haramu" kuilenga miundombinu ya kiraia 

Rais wa Baraza la Ulaya (EU) Antonio Costa amesema katika chapisho lake kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumatatu kuwa kushambulia miundombinu ya kiraia wakati wa vita ni kinyume cha sheria.

Daraja la B1 huko Karaj takriban kilometa 35 kusini magharibi mwa Tehran lililoshambuliwa na kuharibiwa na mashambulizi ya Marekani na IsraelPicha: Atta Kenare/AFP

"Kulenga miundombinu ya kiraia, kama miundombinu ya nishati, ni kinyume cha sheria na haikubaliki. Hili linashuhudiwa katika vita vya Urusi nchini Ukraine na kwengineko, " alisema Costa.

" Raia wa Iran ndio wathirika wakuu wa utawala wa Iran. Pia watakuwa wathirika wakuu wa utanuzi wa operesheni ya kijeshi, " alisisitiza mkuu huyo wa Umoja wa Ulaya katika chapisho lililotolewa baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutishia kuharibu miundombinu ya kiraia nchini Iran ikiwa haitaufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz.

Costa amesema  kuongezeka kwa mashambulizi hakutaleta faida yoyote katika vita hivyo huku akisisitiza kuwa majadiliano pekee ndio yanayoweza kuleta suluhu ya mgogoro uliopo. 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW