1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yakosoa mauaji ya Ali Tabatabai yaliyofanywa na Israel

24 Novemba 2025

Iran imeilaani Israel kwa mauaji ya kamanda mkuu wa kijeshi wa kundi la Hezbollah nchini Lebanon, katika shambulio la tano kufanyika kwenye mitaa ya kusini mwa Beirut.

Libanon Beirut 2025 | Haytham Ali Tabatabai
Haytham Ali Tabatabai ni kiongozi wa ngazi ya juu zaidi wa kundi la wapiganaji wa Hezbollah kuuawa na Israel Picha: Mohamed Azakir/REUTERS

Haytham Ali Tabatabai ni kiongozi wa ngazi ya juu zaidi wa kundi la wapiganaji wa Hezbollah kuuawa na Israel tangu makubaliano ya kusitisha vita kufikiwa Novemba mwaka 2024. Makubaliano yaliazimia kumaliza kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja cha uhasama kati ya Israel na Hezbollah.

Kufuatia tukio hilo, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alisema kuwa nchi yake haitoipa nafasi Hezbollah kujikusanya upya na kuitolea wito serikali ya Lebanon kutimiza wajibu wao wa kuwapokonya silaha wapiganaji hao:

"Saa chache zilizopita, jeshi la Israel lilimuua Ali Tabatabai, kamanda mkuu wa kundi la wapiganaji wa Hezbollah. Tabatabai alikuwa muuaji mkubwa. Mikono yake imejaa damu ya Waisraeli na Wamarekani wengi, kwa hiyo ahadi ya Marekani ya dola milioni 5 kwa atakayemkamata haikuwa ya bure.”

Wakati huohuo, Wizara ya afya ya Lebanon imebainisha kuwa shambulio hilo liliwaua watu wengine watano na kuwajeruhi wengine 28. Hata hivyo, majina ya waliouawa hayajatambuliwa rasmi. Shambulio hilo lilifanyika mtaa wa Haret Hreik ulio na wakaazi wengi kusini mwa mji wa Beirut.

Iran: Mauaji ya kamanda yamekiuka makubaliano ya usitishaji vita 

Iran imeishutumu vikali Israel kwa mauaji hayo, ambapo taarifa ya wizara ya mambo ya nje mjini Tehran, imeyaita "mauaji yaliyofanywa na woga". Iran, ambayo ni mshirika mkubwa wa Hezbollah imesema mauaji ya kamanda huyo yanaonesha wazi ukiukaji wa makubaliano yaliyofikiwa Novemba mwaka jana ya usitishaji vita na yamekiuka uhuru wa mipaka ya Lebanon.

Iran yakosoa mauaji ya Kamanda wa Hezbollah yaliyofanywa na IsraelPicha: Alexander Miridonov/Kommersant Photo/Sipa USA/picture alliance

Kundi la Hezbollah limekiri kuwa wapiganaji wake 4 waliuawa kwenye shambulio hilo. Kulingana na mwandishi wa habari wa shirika la AFP aliyekuwako kwenye eneo la tukio, shambulio hilo lilizilenga ghorofa za tatu na nne za jengo la urefu wa ghorofa 9. Vikozi vya watoaji huduma ya kwanza na zima moto walijitahidi kusaka manusura huku wanajeshi wa Lebanon wakipiga doria. Kwenye barabara iliyoko karibu,uchafu ulitapakaa na magari kadhaa yaliteketea.

Kwa upande wake, Marekani inasisitiza kuwa kamanda huyo wa Hezbollah alisimamia kikosi maalum huko Lebanon pamoja na Syria ambako Hezbollah walimuunga mkono Rais Bashar al Assad wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Wizara ya fedha ya Marekani ilitoa ahadi ya zawadi ya dola milioni 5 kwa atakayekuwa na maelezo kuhusu kamanda Tabatabai. Itakumbukwa kuwa kundi la Hezbollah lilimalizwa nguvu na vita na Israel, vilivyoanzishwa na washirika wao wa Hamas kwenye ukanda wa Gaza mwezi wa Oktoba mwaka 2023 pale mashambulio ya kulipizana kisasi yaliposhuhudiwa na hatimaye kugeuka kuwa mapambano ya moja kwa moja.

Kutokea kipindi hicho, Lebanon imeendelea kupata shinikizo kutoka kwa Israel na Marekani kuwapokonya silaha wapiganaji wa Hezbollah, hatua ambayo imezua hisia mseto. Rais wa Lebanon Joseph Aoun anaitolea wito jamii ya kimataifa kuingilia kati ili kuizuwia Israel kuishambulia.