1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yalaani uamuzi wa OIC kuifukuza Syria

16 Agosti 2012

Uamuzi wa Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu (OIC) kuisitisha uanachama Syria umelaaniwa na Iran, huku wasiwasi ukitanda kuwa mgogoro wa Syria umevuuka mipaka na Umoja wa Mataifa ukisema watu milioni 2.5 wanahitaji msaada.

Mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu Duniani (OIC).
Mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu Duniani (OIC).Picha: AP

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Ali Akbar Salehi, amesema OIC ilipaswa kwanza kuiita Syria na kuisikiliza, kabla ya kufikia uamuzi huo wa kusitisha uanachama wake. Uamuzi wa OIC ulichukuliwa mapema leo asubuhi, baada ya kumalizika kwa mkutano wa dharura uliokuwa umeitishwa mjini Makka kuijadili Syria.

Taarifa ya mkutano huo imesema "OIC inahuzunishwa sana na mauaji ya maangamizi na mateso ya kikatili yanayowafika watu wa Syria."

Licha ya Iran kuhudhuria mkutano huo wa siku mbili, haikuweza kuzuia uamuzi huo, ambao Salehi amesema "unakwenda kinyume na mkataba" wa OIC.

"Kwa maoni yetu Iran, ushirikiano una mantiki zaidi kuliko kusitisha uanachama. Tunapaswa kutafuta njia za kumaliza mgogoro wa Syria, ambapo serikali na upinzani watashiriki kwenye mazungumzo katika mazingira yanayofaa." Amesema Salehi.

Mgogoro wavuuka mipaka

Mkutano huo wa Makka uliitishwa na Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia, ambaye nchi yake inawaunga mkono waasi wanaopigana dhidi ya utawala wa Rais Bashar al-Assad. Tayari hofu zimetanda kwamba mgogoro wa Syria unayashirikisha mataifa na makundi nje ya mipaka ya Syria kwa maslahi na malengo tafauti.

Mabaki ya nyumba zilizoharibiwa vibaya na vikosi vya serikali ya Syria mjini Azaz.Picha: dapd

Utawala wa Saudi Arabia ni wa madhehebu ya Sunni, ilhali wa Syria ni wa madhehebu ya Shia, ambayo ndiyo madhehebu makubwa nchini Iran. Iran imeahidi kuunga mkono kikamilifu utawala wa Assad, ingawa imekuwa ikikanusha kutuma vikosi vyake vya kijeshi na silaha.

Wiki iliyopita, Iran iliitisha mkutano wa mataifa 29 kuizungumzia Syria, ambao ulihudhuriwa na mabalozi na baadhi ya mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa yenye msimamo unaofanana nayo. Saudi Arabia haikushiriki mkutano huo.

Mataifa ya Ghuba yaondoa raia wake Lebanon

Wakati uamuzi huo wa OIC dhidi ya Syria ukitolewa, Saudi Arabia na Qatar zimewataka raia wake kuondoka nchini Lebanon, ambako jana wafuasi wa madhehebu ya Shia walitangaza kuwateka Wasyria 23 na raia mmoja wa Uturuki kulipiza kisasi kwa kukamatwa mfuasi mmoja wa ukoo wa al-Meqdad wa Lebanon na waasi wa Syria.

Mashambulizi dhidi ya kambi ya wakimbizi ya Wapalestina nchini Syria.Picha: picture-alliance/dpa

Saudi Arabia, Kuwait, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu zimetuma ndege kuwachukua raia wao walioko Lebanon. Maofisa wa uwanja wa ndege wa Beirut wameliambia shirika la habari la Ujerumani (DPA) kwamba raia wengi wa mataifa ya Kiarabu walipitisha usiku wa jana uwanjani hapo, wakingojea ndege za kwao kuwarudisha nyumbani. Saudi Arabia imesema imetuma ndege tatu kwa ajili ya kuwaondosha raia wake.

Watu wenye silaha kutoka ukoo wenye huo wenye nguvu sana wa Kishia nchini Lebanon, waliweka vizuizi kwenye barabara kuu ya uwanja wa ndege hapo jana, baada ya kuwateka nyara Wasyria kadhaa wakitaka mtu wao anayeshikiliwa na waasi wa Syria aachiwe huru.

Al-Meqdad watishia kuua mateka

Msemaji wa ukoo huo, Hatim al-Meqdad, amesema waliwateka zaidi ya Wasyria 50 na Mturuki mmoja katika mji mkuu Beirut na mji wa Bonde la Bekaa, mashariki mwa Lebanon. Msemaji huyo ametishia kumuua mateka wa Kituruki masaa machache yajayo ikiwa mtu wao anayeitwa Hassan hakuachiwa huru.

Mpiganaji wa Jeshi Huru la Syria, tawi la kijeshi la waasi, katika mji wa Aleppo.Picha: Reuters

Vikosi vya usalama vya Lebanon, vimeifungua njia ya uwanja wa ndege, ambayo iko kwenye viunga vya kusini ya Beirut, ambako ni ngome ya kundi la Hizbullah, washirika wakubwa wa utawala wa Rais Bashar al-Assad.

Ukoo wa al-Meqdad unaaminika kuwa na mafungamano na Hizbullah, ambayo imekana kutuma watu wa ukoo huo nchini Syria kupigana upande wa serikali dhidi ya waasi. Saudi Arabia, Qatar na Uturuki zinaamikina kuwasaidia waasi, na mara kadhaa zimelaani ukandamizaji wa serikali dhidi ya upinzani.

Jeshi la Syria lashambulia Daraa

Vikosi vya serikali ya Assad hivi leo viliushambulia kwa mizinga na maroketi mji wa Tel-Shihab kwenye jimbo la kusini la Daraa, ikiwa ni mashambulizi ya pili kufanyika ndani ya kipindi cha masaa 24 dhidi ya makaazi ya raia. Zaidi ya watu 40 waliuawa usiku wa kuamkia leo, wakati ndege za jeshi la Syria ziliposhambulia mji wa Azaz, huko Aleppo.

Wakimbizi wa Syria nchini Uturuki.Picha: PHIL MOORE/AFP/GettyImages

Mji wa Tel Shihab ulikuwa nyumbani kwa idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani wa Syria katika siku za hivi karibuni, kwa mujibu wa Shirika la Haki za Binaadamu la Syria lenye makao yake nchini Uingereza.

Hapo usiku, wafuasi hao pia waliziba njia ya kutulia ndege mjini Beirut kuwasha moto matairi, na hivyo kuilazimisha ndege ya Shirika la Ndege la Ufaransa kwenda kutua Cyprus.

Msemaji wa Shirika hilo, ameliambia shirika la habari la Ujerumani, DPA, kwamba walilazimika kuipeleka ndege yao Namba 562 iliyokuwa imebeba abiria 174 nchini Cyprus, "baada ya hali ya usalama kwenye uwanja wa ndege wa Beirut kuzorota."

Tayari mgogoro huo umewageuza raia milioni mbili na nusu wa Syria kuwa masikini wenye uhitaji wa hali ya juu, kwa mujibu wa Mkuu wa Shirika la Misaada ya KIbinaadamu la Umoja wa Mataifa, Valarie Amos, aliyehitimisha ziara yake nchini Syria leo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman