1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yalaani urejeshwaji "usio haki" wa vikwazo vya UN

28 Septemba 2025

Iran imelaani urejeshwaji "usio halali" wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa kuhusiana na mpango wake wa nyuklia, baada ya kuvunjika kwa mazungumzo na mataifa ya magharibi na mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi yake.

Iran | Kiwanda cha nyuklia cha Bushehr
Mwonekano wa kiwanda cha nyuklia cha Bushehr unaonekana kutoka Ghuba ya Uajemi, kusini mwa Iran, Aprili 29, 2024.Picha: Morteza Nikoubazl/picture alliance/NurPhoto

Iran imetoa tamko kali ikisema urejeshaji wa vikwazo hivyo hauna msingi wa kisheria wala kisiasa. Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje, "kufufuliwa kwa maazimio yaliyokuwa yamefutwa ni kinyume cha sheria na hakuna msingi wowote wa kisheria.” Serikali imesisitiza kwamba nchi hiyo "itapigania kwa nguvu zote haki na maslahi ya wananchi wake.”

Vikwazo hivyo vinahusu marufuku ya shughuli zinazohusiana na mpango wa nyuklia na makombora ya masafa marefu. Hatua hiyo ilianza usiku wa kuamkia Jumapili baada ya mataifa ya Magharibi kuanzisha kile kinachojulikana kama "snapback mechanism” chini ya makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015.

Iran inasema uamuzi huo unalenga "kuinyima haki ya maendeleo” na kwamba mataifa yote yanapaswa kutoitambua hali hii waliyoitaja kuwa haramu. Rais Masoud Pezeshkian amesema Marekani ilitoa mapendekezo "yasiyokubalika,” ikiitaka Tehran kuitoa ganda urani yote iliyorutubishwa kwa kubadilishana na ahueni ya muda mfupi ya vikwazo.

Majaribio ya Urusi na China kuchelewesha kurejeshwa kwa vikwazo hivyo hadi mwezi Aprili yalishindwa kupata kura za kutosha kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hatua hiyo ilizusha hasira Tehran na kupelekea Iran kuwaita nyumbani mabalozi wake walioko Ujerumani, Ufaransa na Uingereza kwa mashauriano.

Mabalozi wa Algeria, Urusi, Pakistan na China walipiga kura kuunga mkono kupitishwa kwa rasimu ya azimio kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, Septemba 26, 2025. Hata hivyo, azimio hilo halikupitishwa baada ya kura 9 kupinga, kura 2 kutoshiriki na kura 4 pekee kuunga mkono (Urusi, China, Pakistan na Algeria).Picha: Lev Radin/Pacific Press/picture alliance

Makubaliano ya 2015 na kuvunjika kwa mazungumzo

Makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 (Joint Comprehensive Plan of Action – JCPOA) yalilenga kupunguza kiwango cha urutubishaji wa urani nchini Iran kwa masharti ya kulegezwa vikwazo vya kiuchumi. Lakini Marekani ilijiondoa mwaka 2018 chini ya Rais Donald Trump, jambo lililopelekea mpango huo kuyumba.

Mazungumzo ya kurejesha makubaliano hayo yaliporomoka Juni mwaka huu baada ya Israel na Marekani kushambulia baadhi ya vituo vya nyuklia vya Iran. Mashambulizi hayo yalisababisha vikwazo kuanzishwa upya, yakiwa ya mwisho baada ya miezi kadhaa ya diplomasia yenye msuguano.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), Iran sasa ina akiba kubwa ya urani iliyorutubishwa, hali inayozua hofu kuwa inaweza kutengeneza silaha za nyuklia. Tehran, hata hivyo, inakanusha mara kwa mara madai hayo, ikisema shughuli zake ni kwa malengo ya kiraia pekee.

Mataifa ya Magharibi yanashikilia kuwa Iran haijatekeleza wajibu wake chini ya makubaliano, jambo lililomfanya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul kusema Berlin "haikuwa na chaguo jingine.”

Kwa upande mwingine, Urusi na China zimesema zitaendelea kushirikiana na Tehran, zikieleza kuwa vikwazo hivyo "havina uhalali wowote” na vinaonyesha "siasa za kuburuta miguu za Magharibi.”

Majibu ya kimataifa

Marekani imesema kurejesha vikwazo ni njia ya "kuishinikiza Iran kufanya maamuzi sahihi kwa usalama wa dunia.” Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio aliitaka Tehran kukubali mazungumzo ya moja kwa moja "kwa nia njema.”

Viongozi wa Umoja wa Ulaya pia wamesisitiza kwamba milango ya diplomasia bado ipo wazi. Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, alisema hatua hii "haipaswi kuwa mwisho wa diplomasia,” akisisitiza kwamba suluhu ya kudumu inaweza kupatikana tu kupitia mazungumzo.

Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa Barbara Woodward, akiwa ameandamana na wajumbe wengine wa E3, Balozi wa Ujerumani Ricklef Beutin na Naibu Balozi wa Ufaransa Jay Dharmadhikari, akizungumza na wanahabari kuhusu Iran na silaha za nyuklia nje ya ukumbi wa Baraza la Usalama la UM katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York City, Marekani, Agosti 29, 2025.Picha: Angelina Katsanis/REUTERS

Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kwa pamoja zimesema zitaendelea kusaka makubaliano mapya yatakayohakikisha Iran "haiwahi kutengeneza silaha za nyuklia.”

Hata hivyo, zimesisitiza Tehran ijiepushe na hatua zozote za uchokozi ambazo zinaweza kuzidisha mzozo huu. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameonya kuwa raia wa kawaida ndio watakaoathirika zaidi.

Urusi imechukua msimamo mkali dhidi ya vikwazo, Waziri wake wa Mambo ya Nje Sergei Lavrov akisema vinadhihirisha "siasa za kulazimisha upande mmoja na vitisho vya Magharibi.”

Athari za kiuchumi

Kurejeshwa kwa vikwazo hivyo kunatarajiwa kuathiri vibaya zaidi uchumi wa Iran. Tangu kutangazwa kwa hatua hizo, sarafu ya Iran — rial — imeporomoka hadi kiwango cha rekodi dhidi ya dola ya Marekani, ikiporomoka hadi zaidi ya milioni 1.1 kwa dola moja katika soko la magendo.

Raia wa kawaida tayari wanahisi shinikizo. "Hali ya uchumi ilikuwa ngumu sana, sasa itakuwa mbaya zaidi,” alisema mhandisi Dariush, mwenye umri wa miaka 50 mjini Tehran, akilalamika kuhusu kupanda kwa bei na kuporomoka kwa kiwango cha maisha.

Sekta za mafuta na gesi, ambazo ni uti wa mgongo wa mapato ya taifa, zinaweza kushuhudia kupungua kwa mauzo kutokana na hofu ya washirika wa kibiashara kukiuka vikwazo.

Wachambuzi wanasema hatua hii inaweza pia kuchochea siasa za ndani, ambapo makundi ya kihafidhina yataitumia kama kielelezo cha uonevu wa Magharibi.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) Rafael Grossiamekuwa akisisitiza ulaazima wa maafisa wa shirika hilo kuendelea kukagua mitambo ya nyuklia ya Iran, lakini taifa hilo linamshtumu kunyamazia mashambulizi ya Israel na Marekani.Picha: Joe Klamar/AFP

Wakati huo huo, magazeti ya ndani yametoa mitazamo tofauti: gazeti la kihafidhina Kayhan limesema vikwazo vingerejeshwa hata kama kungekuwa na mazungumzo, huku gazeti la mageuzi la Ham Mihan likihoji iwapo Urusi na China zitadumu na msimamo wao wa sasa.

Kwa majirani wa Iran katika Ghuba ya Uajemi, hofu ni kwamba mzozo huu unaweza kuongeza hatari za kiusalama katika eneo nyeti la usafirishaji wa mafuta duniani.

Mustakabali wa diplomasia

Pamoja na ukinzani huu wote, viongozi wa Ulaya na Marekani wamesema wapo tayari kwa mazungumzo mapya iwapo Tehran itaonyesha nia ya dhati. Waziri Wadephul wa Ujerumani alisisitiza mbele ya Umoja wa Mataifa: "Iran haipaswi kamwe kumiliki silaha za nyuklia, lakini milango ya diplomasia bado ipo wazi.”

Tehran nayo imesema bado iko tayari kwa mazungumzo iwapo tu yatakuwa kwa heshima na usawa. Lakini wachambuzi wanasema changamoto kubwa ni kutoaminiana na tofauti za kisiasa ambazo zimezidi kwa miaka kadhaa.

Kwa sasa, mustakabali wa mpango wa nyuklia wa Iran na nafasi yake katika diplomasia ya kimataifa upo njia panda. Dunia inasubiri kuona iwapo juhudi za diplomasia zitarejeshwa au kama mgongano wa kisiasa na kiuchumi utaendelea kudhoofisha hali ya Mashariki ya Kati.

Chanzo: AFPE, APE, RTRE

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW