1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yalegeza kamba katika msimamo wake

Josephat Charo8 Mei 2007

Mkutano juu ya kuzuia kuenea kwa silaha za kinyuklia unaoendelea mjini Vienna Austria. Hii leo Iran imekubali kulegeza msimamo wake wa kukataa ajenda ya mkutano huo kuhusu njia za kuufanyia marekebisho mkataba wa kimataifa wa kuzuia utapakazaji wa silaha za kinyuklia, NPT.

Balozi wa Iran katika shirika la IAEA Asghar Soltanieh
Balozi wa Iran katika shirika la IAEA Asghar SoltaniehPicha: AP

Hatua ya Iran kulegeza msimamo wake imezuia mazungumzo katika mkutano wa mjini Vienna kusambaratika baada ya mazungumzo hayo kukamwa kwa siku kadhaa. Iran iliitilia guu ajenda hiyo kuhusiana na ibara ya mkataba wa kuzuia utapakazaji wa silaha za kinyuklia, NPT, unaosisitiza haja ya kutii maagizo yote ya mkataba huo. Iran ilihoji kwamba hatua hiyo ni njama inayolenga mpango wa kinyuklia wa Iran na inayaweka kando maswala mengine muhimu katika mkataba huo yanayohitaji kujadiliwa kwa kina.

Iran ambayo inakanusha madai ya mataifa ya magharibi kwamba imekataa kuheshimu mkataba wa NPT na amabayo tayari imewekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa, imekubali kifungu cha maneno kinachosema neno ´kukubali´ lina maana kutekeleza maagizo yote ya mkataba huo. Mataifa 130 yaliyotia saini mkataba wa NPT baadaye yaliidhinisha kwa kauli moja ajenda hiyo na kusababisha kelele za furaha katika jumba la mkutano mjini Vienna.

Pendekezo la mageuzi liliwasilishwa na Afrika Kusini na lililenga kuihakikishia Iran kwamba mjadala ungezishinikiza nchi zinazomiliki mabomu ya nyuklia kuchukua hatua zaidi kutekeleza mkataba wa NPT unaotaka mabomu hayo yaharibiwe, na wala sio tu kuibinya serikali ya Tehran kuhusu mpango wake wa nyuklia. Iran inapinga katakata wasiwasi wa mataifa ya magharibi kwamba inajaribu kutengeneza mabomu ya kinyulia ikitumia sababu ya mpango wake wa kurutubisha madini ya uranium kwa matumizi ya amani.

Iran haijashirikiana kikamilifu na shirika la kimataifa la kuzuia usambazaji wa silaha za kinyuklia, IAEA, tangu uchunguzi wa mpango wake wa nyuklia ulipoanza baada ya habari za utafiti wa nishati ya kinyuklia kufichuliwa mnamo mwaka wa 2002 na Wairan waliokuwa uhamishoni.

Hatua ya Iran kukubali kulegeza kamba katika msimamo wake ina maana kwamba mkutano wa majuma mawili mjini Vienna Austria, ambao unaendelea hadi Ijumaa wiki hii, unaweza sasa kuanza mjadala wa maana kuandaa mikakati ya kufanya mikutano mingine ya kufuatilia swala hilo katika siku za usoni, ili hatimaye mkutano utakaopitisha uamuzi, ufanyike ifikapo mwaka wa 2010.

Mzozo juu ya ajenda uliukwamisha mkutano wa mjini Vienna na kudhihirisha mgogoro mkubwa uliopo baina ya matiafa ya magharibi na Iran kuhusiana na hatua yake ya kukataa kukomesha urutubishaji wa uranium.

Licha ya Iran kukubali pendekezo la Afrika Kusini wanadiplomasia wanatarajia Iran kujaribu kuukwamisha mjadala wa pendekezo la Marekani la adhabu dhidi ya mataifa yatakayojiondoa kutoka kwa mkataba wa NPT. Wairan wenye msimamo mkali wameitaka Iran ijiondoe kutoka wka mkataba huo ikiwa vikwazo dhidi ya serikali ya Tehran vitazidi. Wamesisitiza hakuna haja ya uanachama kama Iran inaadhibiwa kwa mpango unaoruhusiwa na mkataba wa NPT.