1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Iran yamnyonga afisa wa zamani wa wizara ya ulinzi

14 Januari 2023

Iran imesema leo kuwa imemnyonga raia wa Iran aliye pia na uraia wa Uingereza ambaye wakati mmoja alishikilia wadhifa wa ngazi ya juu katika wizara ya ulinzi ya nchi hiyo.

Iran Ex-Vize-Verteidigungsminister Alireza Akbari
Picha: fararu

Hii ni licha ya onyo kutoka kwa jamii ya kimataifa kusitisha adhabu yake ya kifo, na kuongeza hata Zaidi mivutano na nchi za Magharibi wakati kukiwa na maandamano ya kitaifa yanayoitikisa Jamhuri hiyo ya Kiislamu.

Kunyongwa kwa Ali Reza Akbari, mshirika wa karibu wa afisa wa usalama wa ngazi ya juu Ali Shamkhani, kunaashiria mapambano ya madaraka yanayoendelea ndani ya utawala wa Iran wakati ikihangaika kuyadhibiti maandamano kuhusiana na kifo cha Mahsa Amini Septemba mwaka jana.

Soma pia:Iran yawahukumu kifo watu wengine zaidi kufuatia maandamano ya Amini

Kunyongwa kwa Akbari kumezusha hasira kutoka London, ambayo Pamoja na Marekani na wengine zimeiwekea vikwazo Iran kuhusiana na maandamano na hatua yake ya kuiuzia Urusi ndege za kurusha mabomu zisizoruka na rubani ambazo sasa zinaipiga Ukraine.

Ali Akbari alikuwa mshirika wa ShamkhaniPicha: Vahid Salemi/AP Photo/picture alliance

"Hiki kilikuwa kitendo cha kinyama na cha woga, kilichofanywa na utawala wa kikatili usioheshimu haki za binaadamu za watu wake,” amesema Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak.

Waziri wa Mambo ya Kigeni James Cleverly amemuita mkuu wa ubalozi wa Iran nchini Uingereza na kuonya kuwa: "Hiki hakitaenda bila kujibiwa.”

Shirika la Habari la Mizan linalohusishwa na idara ya mahakama ya Iran, imetangaza kunyongwa kwa Akbari bila kusema lini adhabu hiyo ilitekelezwa. Hata hivyo, kulikuwa na tetesi alinyongwa siku kadhaa zilizopita.

Iran ilidai, bila kutoa ushahidi, kuwa Akbari alitumika kama chanzo kwa Idara ya Ujasusi ya Uingereza, inayofahamika kama MI6. Taarifa ndefu iliyotolewa na idara ya mahakama ya Iran ilidai Akbari alipokea kiasi kikubwa cha fedha, uraia wake wa Uingereza na usaidizi mwingine mjini London ili kutoa taaruifa kwa idara ya ujasusi.

Hata hivyo, Iran kwa muda mrefu inawatuhumu wale wanaosafiri ng'ambo au kuwa na mahusiano nan chi za Magharibi kwa kuwa majasusi, aghalabu ikiwatumia kama chambo cha kufanyia majadiliano.

Akbari, aliyekuwa anaongoza shirika moja la kibinafsi, anaaminika kukamatwa mwaka wa 2019, lakini maelezo ya kesi yake yaliibuka wiki za karibuni.

Wale wanaotuhumiwa kwa ujasusi na uhalifu mwingine unaohusiana na usalama wa taifa aghalabu kesi zao hufanywa kwa faragha, ambako mashirika ya haki huwa hawachagui mawakili wao wenyewe na hawaruhusiwi kuona Ushahidi dhidi yao.

Alihudumu kama naibu Waziri wa ulinzi chini ya Shamkhani wakati wa utawala wa mwanamageuzi Rais Mohammad Khatami. Shamkhani kwa sasa ni katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Iran, ambalo ni shirika kuu la usalama la nchi hiyo linaloongozwa na Kiongozi wa juu Ayatollah Ali Khamenei.

Ap, afp, reuters, dpa

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW