1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Iran yamnyonga mtu wa pili kuhusiana na maandamano

Admin.WagnerD12 Desemba 2022

Iran imemnyonga mtu wa pili kuhusiana na maandamano ambayo yameitikisa serikali ya nchi hiyo kwa miezi mitatu sasa, na kukaidi shutuma za kimataifa kuhusu matumizi yake ya adhabu ya kifo dhidi ya waandamanaji.

Öffentliche Hinrichtungen im Iran
Picha: Abedin Taherkenareh/EPA/picture-alliance/dpa

Kulingana na taarifa iliyochapishwa na mtandao wa shirika la habari za mahakama nchini Iran, Mizan, Majidreza Rahnavard alinyongwa hadharani leo Jumatatu katikati ya mji badala ya gerezani.

Taarifa hiyo imesema Rahnavard (ambaye umri wake haujabainika vyema) alihukumiwa kifo na mahakama ya mji wa Mashhad, kwa kuwaua maafisa wawili wa usalama kwa kutumia kisu, na kuwajeruhi watu wengine wanne.

Tukio hilo la kunyongwa kwa Rahnavard limezusha ghadhabu zaidi ulimwenguni. Mnamo Alhamisi wiki iliyopita taifa hilo la Kiislamu lilimnyonga mtu mwengine Mohsen Shekari aliyekuwa na umri wa miaka 23.

Tukio la kwanza la unyongaji kuhusiana na maandamano

Shekari pia alinyongwa kwa kosa la kumshambulia afisa wa usalama wakati wa maandamano. Tukio hilo vilevile lilizusha ghadhabu la lililaaniwa vikali na Ulaya na Marekani.

Maandamano dhidi ya serikali ya Iran yaendelea kupamba motoPicha: AP

Mwishoni mwa wiki, makundi ya kutetea haki za binadamu yalitahadharisha kwamba watu wengine waliokamatwa kuhusiana na maandamano nchini Iran wapo katika hatari kubwa ya kunyongwa.

Iran yamkamata naibu mhariri wa shirika la habari la Fars

Maandamano hayo yalichochewa na kifo cha msichana mwenye umri wa miaka 22  Mahsa Amini mikononi mwa polisi wa maadili kwa madai ya kutovaa Hijab hivyo kukiuka sheria kuhusu  namna wanawake wanavyopaswa kuvaa nchini humo.

Maandamano hayo ambayo mamlaka za usalama zimetaja kuwa vurugu, ni changamoto kubwa kwa serikali tangu mapinduzi ya mwaka 1979 nchini humo. Waandamanaji wamekabiliwa na ukandamizaji ambao wanaharakati wanasema unalenga kuwatia wananchi hofu.

Hukumu za kifo mahakamani

Kabla ya visa viwili vya unyongaji ambavyo tayari vimetekelezwa, mahakama ya Iran ilisema watu 11 wamehukumiwa kifo kuhusiana na maandamano hayo. Lakini watetezi wa haki za binadamu wamesema zaidi ya wengine 12 pia wanakabiliwa na mashtaka ambayo huenda adhabu ikawa ni kifo.

Iran yatoa hukumu ya kifo kwa waandamanaji

Baada ya kisa cha leo, Omid Memarian ambaye ni mchambuzi katika kituo cha Democracy for the Arab World Now (DAWN) yaani Demokrasia kwa Ulimwengu wa Kiarabu Sasa, amesema kesi hizo zinaendeshwa bila kufuata taratibu stahiki na si za haki. Amesema hivyo ndivyo serikali inataka kuyazima maandamano hayo ya nchi nzima.

Masih Alinejad, raia wa Iran aliyeko uhamishoni Marekani, amesema Majidreza Rahnavard ameuawa kwa sababu ya kupinga kuuawa kwa Mahsa Amini, serikali imeamua kuwanyonga waandamanaji. Amezitaka nchi za Umoja wa Ulaya kuwatoa mabalozi wao nchini Iran.

Shutuma za kimataifa

Wiki iliyopita baada ya tukio la kwanza la unyongaji, waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock alisema kitendo hicho kinaonesha dharau isiyo na kikomo kwa maisha ya binadamu.

1,000 washitakiwa kwa kuandamana Iran

Nchi nyingine ambazo zililaani kitendo hicho cha Iran ni pamoja na Uingereza, Canada na Umoja wa Mataifa.

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, zaidi ya waandamanaji 14,000 wametiwa nguvuni nchini Iran.

      (AFPE)

Tafsiri: John Juma

Mhariri: Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW