1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaonya iwapo makubaliano ya nyukilia yatavurugwa

Isaac Gamba
21 Septemba 2017

Rais wa Iran Hassan Rouhani  ameonya kuwa nchi hiyo italazimika kuchukua hatua kali dhidi ya ukiukwaji utakaofanywa kuhusiana na makubaliano yaliyoafikiwa na mataifa yenye nguvu duniani yanayohusu mipango ya nyukilia .

USA Rohani vor der UN-Vollversammlung
Picha: Reuters/E. Munoz

Rouhani ametoa kauli hiyo iliyoonekana kulenga moja kwa moja utawala wa Rais Trump ambao hadi sasa umedumu kwa miezi minane tangu aingie madarakani wakati  kiongozi huyo wa Iran alipouhutubia mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa. Aliongeza kuwa itasikitisha iwapo makubaliano hayo ya nyukilia yatavurugwa na watu wapya katika ulimwengu wa siasa na kuwa dunia itakuwa imepoteza nafasi kubwa. Alisema hata hivyo hata kama hilo likitokea  halitakwamisha  maendeleo ya Iran.

Kauli ya Rouhani inakuja mnamo wakati Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federeca Moghereni akisema kuwa hakuna  haja ya kujadili upya makubaliano yaliyofikiwa kati ya Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani  kuhusiana na mipango ya nyukilia ya Iran kwani kila upande unatekeleza vyema makubaliano hayo licha ya Marekani kusisitiza kutaka yapitiwe upya.

  Moghereni aliyasema hayo wakati alipozungunza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao kilichowashirikisha wawakilishi wa nchi zilizotia saini makubaliano hayo ambacho pia kilihudhuriwa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Iran  Mohammad  Javad Zarif.

Rais Trump ambaye ametishia Marekani kujiondoa kwenye makubaliano hayo iwapo hakutakuwa na uwezekano kuyajadili upya amewaeleza waandishi wa habari kuwa tayari amefikia uamuzi ingawa hakufafanua zaidi.

 Hayo yanajiri wakati nchi 51 zikitia saini mkataba wa kupiga marufuku silaha za nyukilia.  Hatua hiyo ya utiaji saini ilifanyika hapo jana katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

 Hata hivyo hakuna nchi miongoni mwa nchi zinazomiliki silaha za nyukilia au zilizoko katika Jumuiya ya kujihami ya NATO zilizotia saini mkataba huo.

 Mkataba huo wa kupiga marufuku silaha za nyukilia  uliidhinishwa kwa mara ya kwanza Julai 7 na ni mkataba wa kwanza kupiga marufuku silaha za nyukilia.

 

Korea Kaskazini yapuuza vitisho vyaTrump dhidi yake

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong UnPicha: picture-alliance/dpa/R. Sinmun

Wakati huohuo waziri wa mambo ya nje wa Korea Kaskazini  Ri Yong Ho amesema kauli ya kitisho iliyotolewa na Rais Donald Trump kuwa Marekani itaisambaratisha Korea Kaskazini  kuwa ni sawa na "kelele za mbwa anayebweka."  Trump alitoa kauli hiyo  wakati alipolihutubia kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

 Waziri wa mambo ya nje wa Korea Kaskazini Ri Yong Ho aliwaeleza waandishi wa habari mjini New York kuwa itakuwa ni sawa na ndoto ya mbwa iwapo  Trump alikusudia kuitisha Korea Kaskazini na kelele za mbwa anayebweka.   Matamshi hayo ya Korea Kaskazini ni ya kwanza kutolewa na nchi hiyo tangu Trump alipolihutubia baraza kuu la Umoja wa Mataifa ambapo pia alimwita kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un kuwa ni "mtu anayependelea makombora"

Televisheni za Korea Kaskazini zilimuonesha waziri wa mambo ya nje wa Korea  Kaskazini akionekana kuwasikitia wasaidizi wa Trump wakati alipoulizwa na waandishi wa habari juu yamaoni yake kuhusiana na matamshi ya Trump ya kumuita kiongzi wa Korea Kaskazini kuwa ni "mtu wa makombora".

Korea Kaskazini ilifanya jaribio lake la sita la kombora la nyukilia mwezi huu.

Mwandishi: Isaac Gamba/dpae/ape

Mhariri      : Josephat Charo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW