1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaonya kushambulia kambi za jeshi la Marekani

14 Januari 2026

Iran imezionya nchi za kikanda kwamba itashambulia kambi za jeshi la Marekani katika nchi hizo endapo Washington itaishambulia, kufuatia vitisho vya Rais Donald Trump vya kuingilia kati maandamano ya kitaifa.

Iran Tehran 2025 | Rais Masoud Pezeshkian katika mkutano wa mawaziri wa ECO
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian Picha: Iranian Presidency/ZUMA/picture alliance

Afisa wa Iran ambaye hakutajwa jina, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba nchi hiyo imezionya nchi za kikanda kuanzia Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu hadi Uturuki kwamba kambi za kijeshi za Marekani katika nchi hizo zitashambuliwa ikiwa Marekani itailenga Iran na kuzitaka kuizuia dhidi ya shambulizi lolote nchini humo.

Onyo hilo limetolewa huku shirika  la kutetea haki za binadamu la HRANA lenya makao yake nchini Marekani likisema kuwa kufikia sasa, limethibitisha vifo vya waandamanaji 2,403 na maafisa 147 wa serikali. Kwa mujibu wa afisa huyo wa Iran, takriban watu 2000 wameuawa.

Serikali ya Iran imezishutumu Marekani na Israeli kuchochea machafuko hayo pamoja na kuwalaumu watu iliyowaita magaidi kwa kuzua ghasia na kushambulia vikosi vya usalama, misikiti na mali ya umma.

Iran kuharakisha kesi na hukumu dhidi ya waandamanaji

Wakati huo huo, mkuu wa mahakama ya Iran Gholamhossein Mohseni-Ejei , ameashiria leo kuharakishwa kwa kesi na hukumu kwa wale wanaozuiliwa kwa kuhusika katika maandamano nchini humo licha ya onyo kutoka kwa Rais wa Marekani Donald Trump. Matamshi hayo ya Mohseni-Ejei yanakuja huku wanaharakati wakionya kuwa kunyongwa kwa wale wanaozuiliwa kunaweza kutokea wakati wowote.

Rais wa Marekani, Donald TrumpPicha: John Angelillo/UPI Photo/IMAGO

Trump ameonya kuhusu "hatua kali sana" ambazo hazikutajwa ikiwa mamlaka ya Iran itaendelea na vitisho vya kunyongwa kwa baadhi ya waandamanaji, huku Tehran ikitaja onyo hilo la Marekani kuwa "kisingizio cha kuingilia kijeshi" hali nchini humo.

China yapinga uingiliaji wa nje katika mzozo nchini Iran

China imepinga uingiliaji wowote kutoka nje katika masuala ya ndani ya Iran. Haya yamesemwa leo na msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China Mao Ning baada ya kitisho hicho kilichotolewa na Trump.

"Kuhusu hali ya Iran, tumeeleza msimamo wetu mara nyingi. Tunaunga mkono na tunatumai kwamba serikali ya Iran na wananchi wake wanaweza kukabiliana na matatizo ya sasa na kudumisha uthabiti wa taifa. Wakati huo huo, tunapinga uingiliaji wa nje katika masuala ya ndani ya nchi na hatukubaliani na matumizi au tishio la nguvu katika uhusiano wa kimataifa. Tunatumai kwamba pande zote zinaweza kuchukuwa hatua zaidi kukuza amani na utulivu katika Mashariki ya Kati."

Ukandamizaji wa waandamanaji Iran ni wa vurugu

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Noel ‍Barrot, amesema leo kuwa nchi hiyo  inashuku kuwa ukandamizaji dhidi ya maandamano kote nchini Iran ni wa vurugu zaidi katika historia ya sasa nchini humo na kuongeza kuwa lazima usitishwe kabisa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW